Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, leo Machi 03, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bi. Maryam Haji Mrisho ofisini kwake Migombani Zanzibar. Picha na OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameitaka Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar kutekeleza majukumu ya kidiplomasia kwa ufanisi ili kufungua fursa za maendeleo ya Watanzania kwaajili ya kufanikisha matarajio, ndani na nje ya Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa, katika mazungumzo yake na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Bi Maryam Haji Mrisho, aliyewasili hapo kwaajili ya kujitambulisha.
Amesema kuasisiwa kwa Mamlaka za Mambo ya Nje hapa Nchini tangu asili na zama, kulilenga katika kujenga ufanisi wa kidiplomasia kwa upana wake, nje ya Mipaka ya Tanzania, na hivyo kufanikisha matarajio ya wananchi kuzitumia fursa za kujiletea maendeleo.
Mheshimiwa Othman amebainisha fursa hizo ambazo amesema kuwa ni nyingi na zinapatikana ndani na nje ya nchi, zikiwemo huduma za msingi, nafasi za masomo, uchumi, biashara, mifugo, kilimo na uzalishaji wa bidhaa mbali mbali.
Aidha, Mheshimiwa Othman ameitaka Mamlaka hiyo kutengeneza na kuzifungua fursa hizo, ikibidi kupitia Balozi za Nje, hata ziliopo katika Nchi Jirani, mathalan nchini Kenya ambako zipo Taasisi na Jumuiya nyingi zaidi za Kimataifa.
Hivyo, Mheshimiwa Othman ametoa pongezi zake kwa Mkurugenzi huyo Mpya wa Mambo ya Nje Zanzibar, akimtakia kila heri, huku akimuahidi kwamba daima milango ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais iko wazi ili kusaidia, kushauri, kuongoza na kuhamasisha maendeleo ya Nchi.
Naye Mkurugenzi huyo amesema mbali na kuaminiwa kwa nafasi muhimu ya Ukurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, la msingi kunahitajika azma njema ili kufanikisha majukumu ya Ofisi hiyo kwa ufanisi zaidi.
Ili kufikia azma hiyo, Mkurugenzi Bi.Maryam amesema pia ndicho kilichomleta yeye na ujumbe wake kwa Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, kwaajili ya kupata miongozo na taarifa muhimu, ambazo zitasaidia kupatikana kwa fursa na kwa maslahi ya maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
Katika ujumbe wake, Bi Maryam ameambatana na Msaidizi Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar anayehusika na Siasa, Bw. Mohamed Sufiani.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
03/03/2022