Home LOCAL TANZANIA NA ISRAEL KUSHIRIKIANA KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA MAGONJWA YA MOYO KWA...

TANZANIA NA ISRAEL KUSHIRIKIANA KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA MAGONJWA YA MOYO KWA WATOTO

 

 


Na. Catherine Sungura,WAF-Dodoma

Tanzania na Israel  kushirikiana katika kuboresha huduma za Magonjwa ya moyo kwa watoto kupitia Shirika  la SACH linalojishughulisha na huduma za magonjwa hayo kwa watoto nchini humo
 

Akiongea wakati wa kikao hicho leo kilichofanyika jijini Dodoma kati ya Wizara ya afya na Mtendaji Mkuu wa Shirika la huduma za magonjwa ya moyo kwa watoto (Save a Child’s Heart – SACH Bw. Simon Fisher, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kuwa wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika masuala yanayohusiana na huduma hizo hapa nchini.
 

“Kikao hiki kilikua na lengo la kujadiliana maeneo ambayo Wizara ya Afya inaweza kushirikiana na shirika la SACH katika kuongeza idadi ya wataalam watakaopata mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu nchini Israel katika Ubingwa na Ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo kwa watoto”.
 

Aidha, Prof. Makubi amemshukuru Mkurugenzi huyo kwa kutoa huduma za moyo kwa watoto kupitia kambi za matibabu hapa nchini kuanzia mwaka 2015
.

Prof. Makubi alisema kuwa Shirika hilo imekwishatoa tiba kwa watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya Moyo wapatao 130. 
 

Aidha, alimuomba mtendaji huyo kupeleka kambi za matibabu kwenye Hospitali nyingine za Rufaa za Kanda na Mikoa ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
 

“Tunakushukuru kwa kuwezesha Shirika la SACH kwa kuipa kipaumbele nchi ya Tanzania katika kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa wataalam wetu wa hapa nchini kwenye eneo la tiba za magonjwa ya Moyo ikiwemo huduma za upasuaji kwani kupitia huduma hizo Serikali imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipewa rufaa ya kutibiwa nje ya nchi”Aliongeza Prof. Makubi.
 

Licha ya mashirkiano hayo katika upande wa magonjwa ya Moyo kwa watoto na mafunzo Katibu Mkuu huyo hakusita kumuomba Mtendaji huyo  kuongeza idadi ya wanufaika wa mafunzo ya huduma zinazotolewa kupitia Taasisi ya SACH ili kuboresha huduma katika eneo hilo pamoja na kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo kwa wataalam katika huduma za kibingwa za magonjwa ya dharura na huduma kwa wagonjwa mahututi ambapo ujenzi wa miundombinu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya umekamilika.
 

Naye, Mtendaji Mkuu wa SACH BW. Simon Fisher amesema kuwa Shirika lake litaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuimarisha huduma za magonjwa ya Moyo kwa watoto hapa nchini na kuahidi kufanyia kazi maeneo ya ushirikiano yaliyojadiliwa na pande zote mbili wakati wa kikao hicho.
 

Akiwa hapa nchini Mtendaji Mkuu huyo ametembelea  Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo jijini Dodoma kwa lengo la kujionea hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo na pia kupata uelewa juu ya mahitaji ya mafunzo ya Kibingwa na Ubingwa bobezi kwa wataalam wa hospitali hiyo kwenye eneo la huduma za magonjwa ya Moyo kwa watoto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here