Na: mwandishi wetu,Arusha.
Naibu Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo,Pauline Gekul amewataka wasanii nchini kuwa mabalozi wazuri wa wimbo wa Taifa, ili kuhakikisha hakuna mtu anayeweka vionjo vingine nje ya vilivyoasisiwa.
Gekul aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) unaofanyika kwa siku mbili jijini Arusha na kubainisha kuwa kimsingi wimbo huo haupaswi kuchezewa kwa kuingiza vionjo au madogo mengine nje ya vilivyopo.
“Nawaomba nyie muwe mabalozi wa kulinda wimbo wetu huu ambao umeasisiwa na unaonyesha utaofa wetu,haifai kuongizwa madoido mengine ambayo hayaleti utaifa wetu kama ulivyoasisiwa na wasisi wetu, unapaswa kubaki na usajili wake,”alisema
Gekul alisema,fani ya uigizaji inamchango mkubwa kwa Taifa, kwani wamekuwa washiriki wazuri hasa wa kusimama mstari wa mbele kwenye kuhamasisha masuala mbalimbali ya Taifa.
“Kama wakati ule wa vita ya Nduli Idd Amini wasanii walishiriki kutunga nyimbo mbalimbali za kuhamasisha kumpigia adui huyo ili Taifa letu kibali salama,lakini katika vita dhidi ya Uviko-19 na Ukimwi pia tumeona,”alisema naibu waziri huyo.
Aidha,alisema kutokana na umuhimu huo Rais Samia Suluhu kaona umuhimu wa kufufua Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuwapatia zaidi ya Sh.bilioni 1.4 ili kuwania kiuchumi waigizaji nchini.
Alisema kupitia fedha hizo wanaweza kukopa kwa riba nafuu na kuendeleza kazi zao huku wakichangia kukuza uchumi wa Taifa na wao binafsi.
Kuhusu ombi lao la kumuomba Rais Samia awe mgeni rasmi katika kongamano lao,alisema viongozi waandae ratiba rasmi na kufikisha wizarani ili ampigie Rais na anaamini anasikiliza ombi hilo huku akiwataka hao waigizaji kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini ili nao wanufaike nayo.
“Suala lenu mlilonipa hapa la kupunguza kodi alisema Bodi ya Filamu ilikutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwaajili ya kupunguza kodi na tozo za wasanii na linafanyiwa kazi,”alisema
Aliwaasa kudumisha umoja na upendo walionao ili chama chao kistawi na kufanya mambo makubwa zaidi ya kuinua Tania hiyo.
Gekul aliwaomba pia kuhakikisha wanapeleka chama hicho katika kila mkoa ambapo kwa sasa wapo mikoa 22 kati ya 26 licha ya mikoa yote kuwa na wasanii.
Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) Salum Mchoma alisema chama hicho kinawachama hai 36,714 na kusisitiza kuwa wanamahitaji mbalimbali, kwani uigizaji ni rasilimali na kazi yao kubwa kuikumbusha serikali na jamii kuwa sanaa ni muhimu katika uchumi wa nchi.
Alisema Tanzania inazaidi ya wasanii milioni 6 kati yao wasanii milioni 3 wanatokana na kazi za uagizaji lakini hawapo pamoja, hivyo vema serikali kuwakusanya pamoja ili kuwasaidia kutambulika.
Alisema sekta hiyo inamuingiliano wa aina mbalimbali na sekta mbalimbali hivyo alimshukuru Rais Samia Hassan Suluhu kuwakumbuka na kuwakwamua kiuchumi kwa kuwapa Sh,bilioni 1.5 katika mfuko wao, utakaowezesha kukopa kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.
Pia waliomba kutambuliwa na Wizara ya Utumishi na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa)kwani zinashikilia fedha kwaajili ya vijana,ajira na watu wenye ulemavu na kuomba chama hicho kitambuliwe ili wapate fedha za mikopo ili waigizaji wapate maendelo na kujikwamua kiuchumi
“Tunaomba maafisa utamaduni watupokee vivyo hivyo ili tusikwame kimaendeleo pia tunaomba kupunguziwa na kuondolewa kodi na tozo ya kazi kwa wasanii ili tusiwe na mzigo mkubwa wa gharama za kazi zetu,”alisema.
Alisema wanaishukuru Taasisi ya Haki Miliki Tanzania ( Cosota) kwakuwasaidia wasanii pale wanapohitaji msaada wao.
Naye Msemaji wa Yanga na balozi wa kampuni ya GSM,Haji Manara alitoa rai kwa wasanii nchini kutumia misingi ya Azimio la Arusha kwaajili ya kujikwamua kiuchumi kwani hali iliyopo hivi sasa kwa wasanii si ya kuridhisha kutokana na baadhi yao kuwa na majina makubwa lakini uhalisia wa kimaisha duni.