Na: Lucas Raphael,Tabora
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi amewataka watendaji wa serikali wilayani kuhakikisha miradi ya Maendeleo inakamilika kwa wakati na Viwango ili kuleta tija kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa kamati ya siasa ya mkoa wa Tabora ilipofanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Sikonge mkoani hapa.
Alisema kwamba Kamati ya Siasa Mkoa wa Tabora inawajibika kuangalia na kukangua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya zote ilikuona thamani ya fedha ilivyotumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Hassan Wakasuvi aliipongeza Wilaya ya Sikonge kwa ujenzi wa Viwango vinavyotakiwa pamoja na usimamizi mzuri ya miradi hiyo na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na serikali zimetumika vizuri na kuonesha tija kwa wananchi.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Tabora Wakasuvi imekagua ujenzi wa Vyumba 3 vya madarasa ya UVIKO-19 uliogharimu shilingi Milioni 60 katika Shule ya Sekondari Kamagi na kuwapongeza kuwa fedha hizo zimetumika vyema.
Aidha Kamati ilikagua mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi ,Kituo cha Afya Tutuo uliogharimu shilingi Milioni 250, ikiwa ni fedha za tozo za miamala ya Simu mradi ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 25,2022.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge John Palingo aliipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha Mwaka mmoja wa Uongozi wake katika Sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Elimu,Maji na Miundombinu ya Barabara .