Home LOCAL KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPA TANO TMA

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPA TANO TMA

Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) , Mkoa wa Mwanza, Augustino Nduganda (kulia) akifafanua kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, , kuhusu namna rada ya hali ya hewa inavyofanya kazi, wakati kamati hiyo ilipotembelea rada jijini Mwanza.

Muonekano wa rada ya hali ya hewa iliyopo mkoani Mwanza, rada hiyo ni miongoni mwa rada saba ambazo Serikali imeziweka kwenye mpango wa Serikali. Rada hiyo imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso na wajumbe katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mara baada ya kamati hiyo kukagua mradi wa rada jijini Mwanza.

Mhandisi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Benedicto Katole   akifafanua kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso na wajumbe namna rada ya hali ya hewa inavyofanya kazi, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso akishuka kutoka kwenye rada, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa Rada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jijini Mwanza. PICHA NA WUU

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso ameiipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzanai (TMA) kwa maboresho yaliyofanywa na kuufanya utabiri unaotolewa kuaminika.

Akizungumza mara baada ya semina maalum kwa kamati hiyo iliyofanyika jijini Mwanza Mwenyekiti Kakoso amesema usahihi wa utabiri ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaondelea kufanywa na Serikali kwa mamlaka hiyo na kuitaka Serikali kuendelea kuwekeza ili mamlaka iendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojita kwenye utabiri.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya sababu matokeo tunayaona kwa utabiri sahihi lakini pia utoaji wa taarifa umeongezeka na kuwa wa mara kwa mara, hii ni hatua kubwa sana’ amesisitiza Mwenyekiti Kakoso.

Mwenyekiti Kakoso ameiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), kuendelea kuwekeza zaidi kwenye vitendea na maslahi ya watumishi ili kuwapa motisha.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amemuhakikishia Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye Mamlaka hiyo kwani utabiri na shughuli zote zinazofanywa na mamlaka zinaratibiwa kimataifa na ukaguzi hufanywa ili kujiridhisha na huduma zinazotolewa.

“Serikali imeshafunga rada 3 na rada 4 zilizobaki  zimekwisha lipiwa zaidi za asilimia 80 na zitakapokamilika na kuwasili nchini zitainua sana kiwango cha utabiri, hivyo tumejipanga vizuri kwenye kuhakikisha mamlaka inaboreshwa kwenye miundombinu”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Agnes Kijazi ameishukuru Serikali na kusema kuwa rada 4 zilizolipiwa zitaanza kuwasili nchini kuanzia mwezi wa 7 mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu Dkt. Kijazi ameongeza kuwa kwa sasa usahihi wa utabiri baada ya maboresho kwenye miundombinu umepanda na kufikia zaidi ya asilimia 90.

(Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here