Home LOCAL HOTUBA YA MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLAH KATIKA MKUTANO WA SITA WA BARAZA...

HOTUBA YA MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLAH KATIKA MKUTANO WA SITA WA BARAZA LA KUMI LA WAWAKILISHI CHUKWANI ZANZIBAR

Jumla ya maswali ya msingi 139 na maswali ya nyongeza 337 yaliulizwa na kujibiwa pamoja na kujadili Taarifa mbali mbali za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa sita wa Baraza la kumi la wawakilishi.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah katika Hotuba yake wakati akiakhirisha Mkutano wa Sita wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Amesema Mkutano huo uliweza kujadili Taarifa 10 za Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, Taarifa 1 ya Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo Ndogo na Taarifa ya Kamati ya Wabunge watano wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema taarifa zilizowasilishwa zitakuwa chachu kwa Serikali katika kutatua changamoto walizozigundua wakati wa kupitia Taasisi mbali mbali za Serikali, na kuwapongeza wajumbe kwa kuendelea kuisimamia, kuikosoa na kuishauri Serikali katika mambo mbali mbali yanayolenga kuboresha maendeleo ya ustawi wa wazanzibari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa ngazi zote kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa kwa lengo la kupanga vizuri mipango ya maendeleo.
Akigusia uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaagiza Makatibu Wakuu kuwasimamia Watendaji walio chini yao kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi, uadilifu na uwajibikaji kwa kufuata Sheria na Utaratibu wa Utumishi wa Umma ili kuleta tija kwa Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa Nchi kwa kuongeza mapato kupitia njia sahihi ya kutoa na kudai risiti wanapofanya miamala mbali mbali na kuwataka wafanyabiashara kutumia mashine za kieleketroniki kwa lengo la kuboresha huduma zao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Wizara ya Biasahara na Maendeleo ya Viwanda kwa kushirikiana na Taasisi husika kusimamia vyema bei za bidhaa ili kuepuka kupanda bei kiholela hasa katika kipindi kijacho cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

04 Machi 2022

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here