Wadau wanaoshiriki Mafunzo ya watoa huduma katika Mnyororo wa Utalii kupitia Mradi wa UVIKO 19 awamu ya kwanza yanayoendelea Wilayani Rangwa Mkoani Lindi wameiomba Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii kuweka utaratibu wa kuwapelekea mafunzo hayo mara kwa mara ili kuendelea kuwajengea uwezo katika maeneo mbali mbali katika Sekta hiyo.
wakiongea kwa nyakati tofauti walipofanyiwa mahojiano baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuchukua hatua katika kukabiliana na janga UVIKO 19 na kwamba uwepo wa mafunzo hayo kutawajengea uwezo wa kufahamu namna ya kukabiliana na janga hilo.
Hamisi Slim Othman ni mshiriki wa mafunzo hayo, ameeleza kuwa janga la UVIKO 19 limekuwa tishio hasa katika sekta ya Utalii na kwamba ujio wa mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kutokana na uwepo wa wageni wanaoingia nchini na kupata huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Sisi kwa niaba ya Serikali ya Wilaya ya Ruangwa tumefarijika sana kiasi ambacho hatuna cha kuilipa Serikali tumeweza kuona kumbe kuna muingiliano baina ya kuona huduma zetu na hili wimbi la UVIKO – 19 tunakishukuru sana Chuo cha Taifa cha Utalii kutuletea Mafunzo haya tumenufaika sana kwa kufahamu namna gani ya kuwahudumia wageni wanaofika katika maeneo yetu ya kazi” amesema Othman.
Nae mshiriki mwingine wa mafunzo hayo mjasiriamali Lesa Rogers, amesema kuwa amenufaika sana na mafunzo hayo na kwamba elimu hiyo ataitumia kwa kuwaelimisha watu wengine waliokosa fursa hiyo na kwamba amefarijika sana kupata chanjo ambayo inatolewa kwa hiyari katika mafunzo hayo.
“Chuo cha Taifa Cha utalii tunakishukuru kutuletea mafunzo haya mimi kama Mjasiriamali nimenufaika sana kwa kufahamu vitu vingi kuhusu UVIKO 19 hata sasa naweza kuwafundisha na wenzangu namna ya kujikinga na Ugonjwa huu” amesema Lesa Rogers.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ukarimu na Mkufunzi Mwandamizi katika Sekta ya huduma kwa wateja na Mapokezi Jesca Willium amesema kuwa mafunzo hayo yanayoendelea Wilayani Ruangwa yamelenga katika kuwajengea uwezo washiri hao kufahamu mbinu mbalimbali wanazoweza kuzitumia katika kipindi hiki cha UVIKO -19 na kutambua namna ya kutoa huduma zao na kushughulikia changamoto za wateja kwa ujumla.
“Leo tumeendelea na Mafunzo ambapo washiriki wameweza kujengewa uwezo wa mambo mbalimbali yakiwemo masuala ya usafi sehemu zao za kazi na wao wenyewe kama watoa huduma kwa kutambua kuwa ni jinsi gani usafi unavyoweza kuwa suluhisho katika kipindi hiki cha UVIKO 19 na usalama wa chakula kwa ujumla” amesema Jesca.
Mafunzo hayo ya siku tano yanayoratibiwa na Chuo cha Taifa cha Utalii yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa lindi na kuendelea katika mikoa nane ya Tanzania Bara.
PICHA MBALIMBALI ZA WASHIRIKI WA MAFUNZO.