Home LOCAL PROF. KITILA MKUMBO ASHAURI KUPITIWA NA KUPANGWA UPYA MFUMO WA ELIMU NCHINI

PROF. KITILA MKUMBO ASHAURI KUPITIWA NA KUPANGWA UPYA MFUMO WA ELIMU NCHINI

DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameshauri kupitiwa na kupangwa upya kwa mfumo wa Elimu nchini kutokana na mfumo uliopo kwa sasa kuwa na mapungufu mengi.

Akichangia bungeni Januari, 10, 2022 Prof. Kitila amesema mfumo wa Elimu nchini haujasambaa upo “vertical” ambapo ikitokea mwanafunzi amekosea sehemu moja anajikuta ametoka kwenye mfumo hali ambayo husababisha upotevu wa wanafunzi.

Akitoa mchango wake bungeni Prof. Kitila amesema badala ya kushughulikia changamoto za elimu nusunusu ipo haja ya kuupanga mfumo mzima.

“Tupitie na kuupanga mfumo wetu wa Elimu, na jambo hili siyo geni, mwaka 1982 Rais wa awamu ya Kwanza Mwl. Julius Nyerere aliunda Tume ya Makweta ambayo ilipitia mfumo wa Elimu na kuja na suluhisho” Prof. Kitila.

Prof. Kitila amewashauri Mawaziri wamshauri Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume ya Rais itakayopitia mfumo wote wa Elimu na kuupanga upya.

“Jambo hili la kugusa tu mtaala wa msingi peke yake na Sekondari peke yake, haiwezi kututoa tunahitaji Elimu ambayo itafiti Karne ya 21 na ambayo itatupeleka miaka 20 mingine ijayo na huu ni wakati muafaka maana Dira yetu inaisha mwaka 2025 hivyo hii itatusaidia kwenda sambamba na Dira yetu” Prof. Kitila.

Kuhusiana na upotevu wa wanafunzi Prof. Kitila ametolea mfano wahitimu wa kidato cha IV mwaka 2021 ambao walianza shule ya msingi wakiwa 1,500,000 lakini walihitimu kidato cha IV wakiwa 483,820 ambapo zaidi ya watoto milioni 1 walipotea kwenye mfumo wakiwa na umri mdogo.

Amesema hata hao waliohitimu ni 173,000 tu sawa na asilimia 35.8 ya wahitimu wote ndiyo walifaulu kwa Daraja la I -III.

“Mwaka jana Ofisi ya Waziri Mkuu wamefanya utafiti mzuri sana, waliita utafiti wa nguvu kazi ambao ulibaini Milioni 33 ya watanzania sawa na 54% ni nguvu kazi, 16% hawajawahi kwenda shule 65% wameishia darasa la saba na 15% wana elimu ya kidato cha IV” Prof. Kitila Mkumbo

Prof. Kitila amesema ukitazama utafiti huo wa Ofisi ya Waziri Mkuu, utabaini umuhimu wa kuboresha mfumo wa Elimu nchini kwani nguvu kazi iliyopita kwenye mfumo wa Elimu bila stadi zozote ni 96% pekee na 4% ndiyo iliyopita katika mfumo wa Stadi

Previous articleNABII DKT.JOSHUA AITISHA MAOMBI YA SIKU 121 KUMUOMBEA RAIS SAMIA, KUTOKOMEZA MAUAJI
Next articleSERIKALI KUGHARAMIA MATIBABU YA PROF. JAY MUHIMBILI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here