Home LOCAL SERIKALI KUGHARAMIA MATIBABU YA PROF. JAY MUHIMBILI

SERIKALI KUGHARAMIA MATIBABU YA PROF. JAY MUHIMBILI


Na: Sophia Mtakasimba (MNH)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa  kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu  aliyekuwa Mbunge wa Mikumi na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Bw. Joseph Haule (Prof. Jay) anayetibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hadi hapo atakaporuhusiwa kwenda nyumbani.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipofika kumjulia hali msanii huyo  na kuwasilisha salamu za Mhe. Rais.

“Nimefika kuleta salamu za Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini nje ya nchi, amesema kuwa anatambua mchango wa Prof. Jay akiwa Mbunge wa Mikumi lakini pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki hivyo kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu yake hadi hapo ataporuhusiwa kutoka hospitalini  na ninauagiza Uongozi wa Hospitali kuleta bili zote Wizarani kuanzia sasa”, amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema Mhe. Rais anatoa pole za kuuguza kwa familia ya Prof. Jay na pia anamtakia kila la heri katika matibabu anayoendelea nayo, apone haraka ili aendelee na shughuli zake.

Kwa upande wake mke wa Prof. Jay, Bi. Grace Mgonjo amemshukuru Mhe. Rais na kusema kuwa amefanya jambo kubwa sana kwa familia yake na kuongeza kuwa hawajajuta kufuata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili. 

 “Naushukuru sana Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa tangu tulipofika hapa, walitupokea vizuri sana na  hatujawahi kujutia kuwa hapa” amesema Bi. Grace.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amemuhakikishia Waziri Ummy kuwa amepokea maelekezo na atayatekeleza vizuri. 

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utoaji wa matibabu ya kibingwa yanayotolewa kwa Watanzania na kuahidi kutatua changamoto  mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kufanya kazi.

Mwisho

Previous articlePROF. KITILA MKUMBO ASHAURI KUPITIWA NA KUPANGWA UPYA MFUMO WA ELIMU NCHINI
Next articleKUWEPO KWA TAARIFA ZA UONGO KUHUSU AJIRA BENKI KUU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here