Home LOCAL “ONGEZEKO KUBWA LA SARATANI LINACHANGIWA NA MTINDO WA MAISHA” – WAZIRI UMMY...

“ONGEZEKO KUBWA LA SARATANI LINACHANGIWA NA MTINDO WA MAISHA” – WAZIRI UMMY MWALIMU



Na: WAF – Dodoma.

Katika  kipindi cha miaka kumi nchi imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani unaochangangiwa na mtindo wa Maisha usiozingatia lishe Bora ikiwa ni Pamoja na  kutokufanya mazoezi.

Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu leo jijini Dodoma wakati akitoa tamko la siku ya saratani duniani ambapo amesema sababu nyingine kuwa ni unene ulikithiri,matumizi ya tumbaku na bidhaa zake,matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda,matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi.

Waziri Ummy amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali imeimarisha huduma za kibingwa katika hospitali 6 za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya Uchunguzi na Tiba kwa kuongeza wataalam, miundombinu pamoja na Vifaa Tiba.

Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018, zikionyesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 42,060 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 hufariki kutokana na ugonjwa huo. 

Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa katika kila watu 100,000, watu  76 hugundulika kuwa na ugonjwa  wa Saratani.

Katika taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume (21%), Saratani ya Koo (11.8%), Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%)  na kwa upande wa wanawake saratani zinazowaathiri zaidi ni pamoja na Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8%).

Waziri Ummy ameweka wazi kuwa saratani ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote watoto, watu wazima, wanawake na wanaume ambapo takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani kila mwaka ambao ni sawa na takribani asilimia 50.

Aidha, zaidi ya watu  ya millioni 43.8 wanaishi na saratani duniani.  “Kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la saratani linakadiriwa kuongezeka na idadi ya wagonjwa wapya kufikia  milioni 24 ifikapo mwaka 2035, huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea kama Tanzania”.

Vile vile ameeleza kuwa takwimu kutoka kwenye kanzi data zilizo anzishwa kwa Kanda , zinaonesha kwamba wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma  ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongzeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa.

“Ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi”, amesisitiza Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema  katika kipindi cha  miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi.     

“Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya”.

“Kwa wale ambao  wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha,”ameongeza Waziri Ummy.

Hata hivyo amesema kuwa Tanzania imetunga Sheria mbalimbali , miongozo na mikakati ya udhibiti wa vihatarishi ili kuweza kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambapo karibu theluthi moja ya Saratani zinaweza kutibika endapo mgonjwa atabainika mapema.

Serikali ya awamu ya sita  imehakikisha huduma za kinga na matibabu ya saratani zinapatikana nchini ambapo vituo vya uchunguzi na matibabu ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi zaidi ya 800 vimefunguliwa nchi nzima kuanzia kwenye ngazi ya Zahanati hadi kwenye ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda. 

“Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 51.5 ikilinganishwa na vituo 350 vilivyokuwepo kwa mwaka 2015. Mafanikio haya yamepelekea serikali kuweza kutoa huduma za uchunguzi za saratani ya mlango wa kizazi kwa Jumla ya wanawake 513,375 sawa na ongezeko mara nne idadi ya wanawake 127, 188 waliopatiwa huduma hizo mwaka 2015,”.

MWISHO.

Previous articleMHE. MARY MASANJA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 45 YA CCM BUTIAMA
Next articleWAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUHAMASISHA CHANJO YA IVIKO 19
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here