Home LOCAL MIPANGO YA KAZI ZA NGO ZIENDANE NA MIPANGO YA KISEKTA: DKT. SICHALWA

MIPANGO YA KAZI ZA NGO ZIENDANE NA MIPANGO YA KISEKTA: DKT. SICHALWA


Na: WA-KARATU.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwa ameelekeza mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO) kuhakikisha mipango au afua wanazotekeleza katika ngazi ya jamii ni lazima iendane na mipango ya Kisekta ili kuepuka mkanganyiko katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Dkt. Sichalwe ametoa maelekezo hayo leo Januari 31, 2022 alipofungua Kikao na Wadau kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la EGPAF kilichofanyika katika Mkoa wa Manyara Wilayani Karatu.

“Wakati mnatengeneza mipango yenu na shughuli mtakazofanya ni lazima mhakikishe shughuli hizo au mipango hiyo inaendana na mipango ya Sekta ya Afya ili kwa pamoja mipango hiyo isaidie kuongeza kasi ya kuboresha utoaji wa huduma katika jamii.” Amesema Dkt. Sichalwe.

Kwa upande mwingine Dkt. Sichalwe amesema, Bado ipo haja ya kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, licha ya hatua kubwa ambayo Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeendelea kufanya hasa katika kuibua wagonjwa hao

Amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imepiga hatua katika kufikia 95% kuibua wagonjwa wa HIV, 95% kuwaanzishia matibabu na 95% kuhakikisha wanafubaza virusi vya UKIMWI, huku jitihada hizo zikiendelea ili kuhakikisha ifikapo 2030 ugonjwa wa UKIMWI unatokomezwa nchini.

Aidha, Dkt. Sichalwe ameelekeza kuongeza kasi katika kutoa Elimu ya umuhimu wa kujua hali ya maambukizi kwa wananchi hususan kwa kundi la Wanaume ambalo bado lipo nyuma katika kutambua hali zao za maambukizi.

Hata hivyo, amesisitiza kuongeza ubunifu katika kuwafikia wanaume katika jamii kwa kutembelea katika maeneo wanayoshiriki shughuli mbalimbali ikiwemo katika maeneo ya shughuli za michezo na uchumi.

Mbali na hayo amewataka EGPAF na Wadau wengine kuendelea kutoa Elimu ya uhamasishaji wa Chanjo ya UVIKO 19 kwa Wananchi, hasa makundi maalumu kama watu wanaoishi na VVU pamoja na wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB).

Kwa upande mwingine, Dkt. Sichalwe amesisitiza katika huduma zote zinazotolewa na Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali ni lazima yazingatie ubora wa huduma ili wananchi wanufaike na huduma hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here