Home BUSINESS KAMATI YA SERA YA FEDHA YA BENKI KUU YARIDHISHWA NA MWENENDO MZURI...

KAMATI YA SERA YA FEDHA YA BENKI KUU YARIDHISHWA NA MWENENDO MZURI WA UCHUMI

Na: Mwandishi Wetu.

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanya kikao chake cha kawaida cha 218 Januari 31,2022, na kupitia utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema kwamba  Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo mzima wa uchumi, na kuidhinisha Benki kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi, ili kusaidia kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi. 

Msimamo huu umechukuliwa kwa kuzingatia matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5. 

Aidha imeridhishwa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara, uliokua kwa wastani wa asilimia 4.9 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2021. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchimbaji madini, viwanda na usafirishaji. 

Aidha, Kamati ilibaini ongezeko la mfumuko wa bei kufikia asilimia 4.2 mwezi Desemba 2021 kutoka asilimia 3.8 mwezi Julai 2021, kutokana na changamoto za ugavi, hata hivyo mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5. Uchumi wa Zanzibar umekua kwa kasi ya kuridhisha kufikia asilimia 8.8 katika robo ya tatu ya mwaka 2021, ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho 2020, kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, hususan utalii.

Mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ukichangiwa na bei zisizo za vyakula, hata hivyo umeendelea kubaki ndani ya lengo la chini ya asilimia 5.

Kamati imeridhishwa na kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 7.8 na asilimia 10 mwezi Novemba na Desemba 2021, mtawalia, kutoka chini ya asilimia 5 kwa sehemu kubwa ya mwaka 2021. Mwenendo huu ni sambamba na lengo la ukuaji wa asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/22.

Ukuaji huu ulichangiwa na utekelezaji wa sera ya fedha yenye kuongeza ukwasi katika uchumi; utekelezaji wa hatua za ziada za kisera zinazolenga kuchochea 

utoaji wa mikopo na kushusha viwango vya riba; pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kufuatia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia. Sekta ya nje imeendelea kuimarika kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19, ikidhihirishwa na kurejea kwa shughuli za utalii. 

Akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 6.4, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 6.6. Utekelezaji wa bajeti ya Serikali uliendana na matarajio 

kutokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na misaada na mikopo kutoka nje.

Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa ndani pamoja na wa dunia, na hivyo matarajio ni kuwa malengo ya sera ya fedha yaliyowekwa katika Tamko la Sera ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2021/22 yatafikiwa.

Gavana

Benki Kuu ya Tanzania

BENKI KUU YA TANZANIA

16 Barabara ya Jakaya Kikwete

S. L. P. 2303

40184 DODOMA

TANZANIA

Simu: +255 26 2962586

Previous articleMIPANGO YA KAZI ZA NGO ZIENDANE NA MIPANGO YA KISEKTA: DKT. SICHALWA
Next articleWATU WANAOKUTWA NA UTI MARA KWA MARA WANAWEZA KUWA NA MAWE KWENYE FIGO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here