Amesema habari zitakazoandikwa zikianisha fursa mbalimbali zinazoonyesha fursa zinazopatikana katika kilimo cha Parachichi Nyanda za juu Kusini zitahamasisha wakulima wengi kujiingiza kwenye zao hilo na hatimaye kujikwamua kiuchumi na kuisaidia Taifa kupata fedha za kigeni.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mbeya, Dk. Nicholaus Kessy kwa niaba ya Naibu Gavana wa (BoT) nchini, Bernard Kibesse wakati akifungua semina kwa Wahariri na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini inayofanyika katika tawi la (BoT) jijini Mbeya.
“Semina hii imejikita kuwafundisha wanahabari kuwa wabobezi wa habari za Uchumi, fedha na biashara kwa sababu wanahabari wakibobea katika eneo hilo wataweza kuandika kwa weledi habari zinazohusu sera mbalimbali za fedha pamoja na kuchambua kupitia vipindi, na makala zinazoeleza majukumu ya benki kuu Tanzania. ,” amesema Dk. Kessy.
Ameongeza kuwa wanahabari wanapaswa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana hususani Mikoa ya Nyanda za juu kusini ikiwamo vivutio vya uatlii na kilimo ili kuwavutia wawekezaji na watalii kutembelea Hifadhi za Taifa kama vile Kitulo, Ruaha, Katavi , Ziwa Ngosi na maeneo mengine yenye kuvutia.
Naye, Kaimu Meneja wa Mahusiano na Itifaki kutoka Benki ya Tanzania (BoT), Vicky Msina amesema semina inayotolewa kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha inalenga kuwajengea uwezo kuchambua na kuandika habari kwa weledi zinazohusu majukumu ya benki.
Msina amesema miongoni mwa mambo wanayofundishwa wanahabari ni kutambua matumizi ya lugha za kifedha ili kuwasaidia wanahabari kuandika habari zitakazoeleweka kwa jamii.
“Hii ni semina ya tisa tangu kuanza kwa utaratibu huu, tumeona manufaa makubwa baada ya kuwapatia wanahabari mbalimbali nchini kuhusu masuala mbalimbali yanayofanywa na Benki kuu ya Tanzania pamoja na masuala mengine yanayohusu biashara na uchumi,” amesema Msina.
Picha ya Pamoja