Home LOCAL WAZIRI BASHUNGWA KUWAPIMA WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI NCHINI KATIKA UKUSANYAJI MAPATO.

WAZIRI BASHUNGWA KUWAPIMA WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI NCHINI KATIKA UKUSANYAJI MAPATO.

Na: Maiko Luoga Njombe.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa  TAMISEMI Mhe, Inocent Bashungwa amesema moja ya vipimo vya utendaji vitakavyotumika kwa wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini ni uwezo wa kukusanya mapato na usimamizi wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo.

Waziri Bashungwa amesema hayo Januari 21/2022 wakati akizungumza na watumishi wa mkoa wa Njombe baada ya kuwasili mkoani humo kwaajili ya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutumia nafasi hiyo kuwataka Viongozi wa Halmashauri kuongeza kasi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

“Haya ni maelekezo kwa nchi nzima, moja ya vigezo tutakavyotumia kuwapima Wakuu wa wilaya na wakurugenzi ni utendaji katika ukusanyaji wa mapato pia usimamizi na uadilifu katika kusimamia fedha zinazoenda kwenye miradi ya maendeleo” amesema Mhe, Bashungwa.

Aidha amesema wizara imeandaa mpango wa kuanzisha vituo vya kupokea kero za wananchi katika mikoa ili kurahisisha utatuzi wa kero hizo tofauti na njia zinazotumika sasa.

“Nimetoa maelekezo Ofisi ya Rais TAMISEMI wizarani kuhakikisha watumishi na kompyuta za kutosha zinakuwepo ili Mtanzania yeyote alipo hata kwenye Kitongoji akiona kuna mambo hayaelewi kwenye mradi uliopo katika eneo lake apige simu tutumie vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia, kuchunguza na kuchukua hatua” Mhe, Bashungwa.

Akitoa taarifa ya maendeleo Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya ameshauri Serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI kushughulikia changamoto ya vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma za Afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto mkoani hapo.

“Vifo vya akina mama ambavyo hutokana na changamoto za uzazi katika mkoa wetu vimepungua, kipindi cha miezi sita iliyopita tulikuwa na vifo kumi na moja lakini kati ya hivyo saba vilitokana na changamoto ya UVIKO, ukitoa hivyo maana yake tulikuwa na vifo vinne vya uzazi ukilinganisha na vifo zaidi ya kumi na tano tulivyokuwa navyo ndani ya miezi sita ya awali” Mhandisi Rubirya Mkuu wa mkoa wa Njombe.

Mbunge wa Ludewa Mhe, Joseph Kamonga kwa niaba ya wananchi wa Jimbo hilo amemwomba Mhe, Waziri Bashungwa kutazama na kutatua changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara za Vijijini ambazo mara nyingi hutumika kusafirisha mazao ya kilimo.

“Wilaya yetu ya Ludewa inajishughulisha sana na kilimo kuna mazao ya mbao, mahindi kwa wingi, korosho upande wa ziwa nyasa na mazao mengine ikiwemo viazi, hivyo magari mengi yenye uzito mkubwa yanapita huko vijijini, lakini Bei ya mazao inakuwa ya chini sana kutokana na ubovu wa barabara wanunuzi hutumia kigezo hicho kuwadhurumu wananchi” alieleza Mhe, Joseph Kamonga.

Wananchi mkoani Njombe wamesema wanaamini ziara ya Waziri wa TAMISEMI Mhe, Inocent Bashungwa aliyoifanya mkoani humo itazaa matunda kwakuwa atapita kuona na kukagua baadhi ya miradi inayoendelea mkoani Njombe pamoja na kuimarisha ari ya utendaji kwa watumishi wa Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here