Na: WAF – Moshi, Kilimanjaro.
Viongozi wa Dini na Kimila wa Mkoa wa Kilimanjaro wameombwa kushirikiana na Serikali katika kuelimisha wananchi kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na kutoa hamasa ya chajo.
Ombi hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Dini na Kimila katika Semina maalum iliyowakutanisha pamoja na wataalam wa afya katika Mkoa wa Kilimanjaro.
“Dawa au chanjo yoyote inapoingia nchini ni lazima ipimwe kwanza na taasisi zetu za hapa nchini ili kujihakikisha usalama kwa wananchi, hivyo niwaeleze kuwa chanjo zote zinazotumika kwa ajili ya UVIKO-19 zimehakikiwa kuwa ni salama na hazina madhara” amesema Dkt. Mollel
Dkt. Mollel amesema kuwa chanjo ni salama kwa binadamu na inaokoa maisha huku utafiti wa sasa ukionyesha kuwa watu waliochanjwa hata wakiambukizwa tena corona hawapati madhara makubwa kama ambao hawajachanja.
Ameendelea kusema kuwa upo uvumi kwamba Serikali ilikuwa inakataa chanjo lakini leo imebadilika na kusema chanjo ni salama, akijibu hoja hiyo Dkt. Mollel amesema; mojawapo ya
Kazi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Usalama wa watanzania kwanza. Chanjo ilipotangazwa imepatikana, Tanzania ilitaka kujiridhisha kwanza kwa kiwango cha kutosha kabla ya kukubali kutumika kwa Watanzania.
Aidha, Dkt. Mollel ametoa rai kwa wananchi kupitia viongozi hao kuendelea kufuata taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya kwa ajili ya kujikinga dhidi ya UVIKO-19 pamoja na kujitokeza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupata chanjo ya UVIKO-19.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Stephen Kagaigai amesema kuwa Mkoa huo umeathiriwa sana na ugonjwa wa UVIKO-19 uliochagizwa na mwingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali hivyo kusababisha kasi kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huo kutoka nje ya nchi.
Mhe. Kagaigai amesema kuwa Ili Mkoa huo uwe salama, ni lazima asilimia 60 ya wananchi katika Mkoa wa Kilimanjaro sawa na watu zaidi ya milioni moja na laki mbili wawe wamepata chanjo ya UVIKO-19 itakayowasaidia wananchi kuongeza kinga dhidi ya ugonjwa wa corona.
“Naomba Viongozi wa Dini naQ wa Kimila mliopo hapa mtusaidie kwenye maeneo yenu, tunafahamu kuwa mna watu wengi, ushawishi mzuri na mkubwa kabisa twendeni tukawaelimishe wananchi na kutoa hamasa ya chanjo ya UVIKO-19” ameomba Mhe. Kagaigai.
Mwisho