NA: MWANDISHI WETU.
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kupitia Hifadhi yake ya Serengeti limeboresha shughuli za Utalii na kuongeza uzoefu kwa watalii wanaotembelea kwa kujenga vibao maalumu (interpretative panels) vyenye maelezo katika sehemu hizo za vivutio.
Kwa mujibu wa Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi na Mawasiliano kutoka TANAPA, SAC CC. Pascal Shelutete amesema kuwa, vibao hivyo maalum vitakuwa ni chachu kwa wageni wanaotembelea hifadhini kujionea vivutio vya kiutamaduni vilivyopo ndani ya eneo la Moru katika Hifadhi hiyo ya Serengeti.
“Sambamba na Watalii kupata fursa ya aina yake ya kuona Faru weusi ndani ya eneo la Moru pekee, watalii watapata maelezo ya vivuvito vya kitamaduni kupitia vibao hivyo hivyo.
Kwani uboreshaji huu ni wa kipekee kupitia vibao hivyo vilivyojengwa kwa ubora mkubwa vikiwa na maelezo ya maisha ya kabila la Dorobo na Masai namna walivyoishi na wanyamapori, matambiko yao na wanyama walioheshimika zaidi na kwanini.” Alisema SAC CC Pascal Shelutete.
Na kuongeza: “Karibu Serengeti kwa uzoefu wa kipekee ndani ya eneo la Moru ambapo utafurahia kuona faru weusi na historia na tamaduni za watu wa kale kama ‘Masai rock paints’, ‘Gong rocks’ na Historia ya wanyama adimu aina ya Faru weusi.” Alimalizia SAC CC Pascal Shelutete.
Mwisho.