Na: WAF, Kigoma.
Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel ameagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizopo pembezoni mwa nchi kuweka utaratibu endelevu wa kuwa na kambi za kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Dkt Mollel ametoa agizo hilo leo akiwa wakati wa uzinduzi wa Kambi ya Huduma za Kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni Kigoma na kujionea hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Huu utaratibu wa madaktari wetu bingwa kutoka hospitali za kibingwa kuwafuata wananchi waliopo kwenye Mikoa iliyopo pembezoni na kuhudumiwa huko utakuwa ni utaratibu endelevu na kwa maeneo yote ya pembezoni katika nchi yetu” amesema Dkt. Mollel
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuboresha Sekta ya Afya nchini kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za afya, ununuzi wa vifaatiba pamoja na kusomesha watalaam wa afya ndani na nje nchi huku akikiri kuwa bado tuna changamoto ya uhaba wa wataalam wa kibingwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Dkt. Mollel amesema kuwa kambi hizo za madaktari bingwa kuwepo kwenye maeneo hayo ya mbali kutawasaidia wananchi kuokoa fedha ambazo wangezingetumia kwenda umbali mrefu kufuata huduma za tiba.
Aidha amepongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kusimamia vyema ujenzi wa miundombinu inayoendelea kujengwa katika Hospitali hiyo ambayo itawawezesha wataalam hao bingwa kuweza kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
Katika kukabiliana na uhaba wa wataalam bingwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo pembezoni mwa nchi, Dkt. Mollel ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Afya kurejea upya uwiano wa wataalam bingwa katika Hospitali za Umma nchini na kufanya uhamisho wa watalaam wachache ili wahamie katika Hospitali ya Maweni na kurahisisha utoaji endelevu wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Simon Chacha amesema Mkoa huo umekuwa ukitoa rufaa za tiba kwa wagonjwa kutoka Mkoa huo kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Mwanza au Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Aidha Dkt. Chacha amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa fedha kiasi cha Tsh Milioni 619 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji lenye vyumba vitatu ambalo limekamilika na huduma tayari zimeanza kutolewa katika Hospitali ya Maweni.
Amesema kuanza kutolea kwa huduma katika jengo hilo kutaongeza huduma za kibingwa za upasuaji zinazotolewa katika Hospitali hiyo.
Awali akizungumza, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni Kigoma, Dkt. Stanley Binagi amesema kupitia kambi hiyo iliyoanza kutoa huduma tarehe 24/1/2022 juma la wateja 914 wameweza kupata huduma za tiba za kibingwa katika kambi hiyo iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni.
Aidha Dkt. Binagi amesema kuwa Hospitali hiyo imeanzisha huduma za kibingwa za magonjwa ya ndani, mifupa, ICU pamoja na kusafisha damu ambazo zinapatika Hospitalini
Naye Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Mhe. Kirumbe Shabani Nge’nda ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuja na kambi hiyo ambayo itawasaidia wananchi wa Mkoa wa Kigoma kupunguza gharama ambazo wangetumia kufuata huduma za kibingwa katika Mikoa ya mbali.
Mwisho.