Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
Na: WMJJWM Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainabu Chaula amekabidhiwa rasmi Ofisi ya Wizara na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye kwasasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuiunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Wizara Dkt. Zainabu Chaula, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.
“Kila mmoja hapa ana karama yake, sasa tuunganishe hayo Maarifa ya mtu mmoja mmoja tutembee pamoja” Dkt. Chaula
Ameongeza kuwa, kiongozi ni wasifu katika eneo analofanya kazi na kuleta matokeo chanya kwenye eneno la utekelezaji wa majukumu yao hivyo, ni vyema watahakikisha wanatumia vipawa vyao kusadia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
“Tutumie ujuzi na uwezo wote tulionao kuhakikisha tunasaidiana katika kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na ufasaha ili kuhakikisha yanaleta matokeo chanya” alisema Dkt. Zainabu Chaula.
Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu amewashukuru Watumishi wa Wizara hiyo Mpya kwa ushirikiano waliompa wakati akitekeleza majukumu yake na kuwaasa kuendelea kuwapa ushirikiano viongozi wapya katika utekelezaji wa majukumu waliyopewa na Rais.
“Nawaahidi nitaendelea kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi ili tuendelee kumsaidia Rais katika kutatua changamoto za kimaendeleo “ alisema Dkt. Jingu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, amewaasa watumishi kupendana na kushirikiana kwa pamoja katika majukumu yao ili kuwasaidia Viongozi kuendeleza jukumu la Maendeleo.
Mapema Januari 8, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, aliunda Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum na kisha kuteuwa Viongozi wakuingoza Wizara hiyo.
MWISHO.