Na: Tito Mselem, Morogoro,
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka wachimbaji wa madini wa vijiji vya Lubungo Kata ya Mikese na Maseyu Kata ya Dwata wilaya ya Morogoro kuachana na migogoro katika maeneo yao ya uchimbaji na badala yake washirikiane katika shughuli zao cha uchimbaji madini.
Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo alipotembelea vijiji hivyo vyenye shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu ambapo amesema migogoro baina ya wawekezaji wa madini na wachimbaji wadogo mkoani Morogoro inatakiwa kuisha kwa wao wenyewe kushirikiana kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizopo na kueleza kuwa migogoro hiyo hailipi na badala yake inazidi kuwarudisha nyuma na kukimbiza maendeleo kwenye maeneo yao.
Aidha, Dkt. Biteko amesema mapinduzi katika Sekta ya Madini yameongezeka katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo mapato yatokanayo na madini kuongezeka.
Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amesema kwa sasa wawekezaji kutoka nje wanakuja kwa wingi kutokana na kufunguliwa kwa milango ya nchi ambapo hivi karibuni inchi ilishuhudiwa kusainiwa kwa mikataba mikubwa ya uchimbaji madini.
Pia, Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wa madini nchini wanamuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na namna alivyoweza kufanya ushawishi wa kuwaleta wawekezaji baada ya kwenda nje ya nchi na kufanya mazungumzo na viongozi wenzake.
“Mimi na wenzangu kutoka Wizara ya Madini tunaona, juzu juzi tumesaini mikataba mingi ya uchimbaji mkubwa wa madini ambayo hatujawahi kutokea ila katika kipindi cha Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan imetokea,”amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema kwa sasa Serikali inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa madini na kuzifungamadisha sekta zingine katika fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amempongeza Dkt. Biteko kwa kutembelea wilaya hiyo na kumuahidi kuyafanyia kazi maagizo yake yote atakayo yatoa.
Msani amesema uongozi wa wilaya yake utasimamia Sekta ya Madini kikamilifu pamoja na kutatua kero zitokanazo na sekta hiyo sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo ambao licha ya madini kuwepo katika maeneo yao lakini bado wanaishi katika nyumba za matope na majani.