Waziri wa Nchi (OR) Tawala za Mikoa na Idara maalum za SMZ Mh.Masoud Ali Mohammed akikata utepe kuzindua gari za kisasa za kubebea taka ngumu kwaajili ya kuimarisha usafi ,hafla iliyofanyika viwanja vya kumbukumbu za mapinduzi Kisonge.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ.Mheshimiwa Masoud Ali Mohamed amewataka wananchi kuziunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha mji unakuwa safi.
Kufanya hivyo kutaisaidia Zanzibar kuwa na haiba nzuri ambayo itaweka ustawi bora na kivutio kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mifuko maalum ya kuhifadhia taka pamoja na gari za kisasa za kusafirishia zilizotolewa na Kampuni ya Vigor huko katika Uwanja wa Mapinduzi Square Kisonge .
Amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt,Husein Mwinyi ametoa rai yenye dhamira njema kuhakikisha mji unakuwa safi hivyo iko haja ya wananchi kushirikiana kwa pamoja kudumisha usafi katika maeneo yao.
Aidha alisema Kampuni ya Vicline itashirikiana na Serikali kuondoa changamoto iliyopo ya kusambaa taka taka katika mji jambo ambalo linapoteza haiba na ustawi wa mji .
Alifahamisha suala la kujenga nchi sio la serikali pekee bali ni jukumu la wananchi wote hivyo iko haja ya mashirikiano ili kuhakikisha azma iliokusudi inafikiwa.
Waziri Masoud alisema licha ya taka kuna uchafuzi wa mazingira ya kubandika matangazo mengi kiholela bila ya kufuata utaratibu kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa alisema bado mji haujaridhisha hasa katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambao ni jicho la Zanzibar hivyo sheria ndogo ndogo zipitiswa kwa kutoa faini kwa wanaochafua mji .
Alisema ni vyema jamii kuimarisha mji kwa kupanda bustani mbali mbali katika maeneo yao ili kuengeza uzuri wa mji wa Zanzibar.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa Mjini, Ali Khamis alisema Baraza la Manispaa kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa taka kumetokana na gharama kubwa ya uendeshaji, uchakavu na uwezo mdogo wa vifaa vya ukusanyaji wa taka pamoja na uchache wa rasilimali watu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kampuni Vigor ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Taufik Salum Turkey amesema kampuni hiyo inamkakati wa kuzisarifu taka kwa lengo la kubuni miradi na kuzalisha viwanda vidogo vidogo vya vyakula vya kuku majongoo mbolea pamoja na karatasi jambo ambalo litasaidia kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Akitoa wito kwa jamii alisema usafi ni jukumu la wote hivyo tushirikiane tuimarishe mji kwa pamoja na Kauli Mbio ya Uzinduzi huo ni Weka Mji Safi kwa Utalii bora Zanzibar.