Home LOCAL MAHAFALI YA 15 CHUO KIKUU MUHAS YAFANA, WANNE WAPATA (PhD)

MAHAFALI YA 15 CHUO KIKUU MUHAS YAFANA, WANNE WAPATA (PhD)



Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete akiwatunuku wahitimu wa Shahada ya uzamivu (PhD) kwenye Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam, leo.


Wahitimu wanne walopata Shahada ya juu ya Uzamivu ya udaktari wa Falsafa (wa kwanza kushoto waliokaa viti vya mbele), ni Mourice Mbunde,(kulia) ni Mboka Jacob, (waliokaa viti vya nyuma), ni Baraka Samweli (kulia),na Zuhura Idd Kimera (kushoto),


Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza kwenye Mahafali hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo hicho Nijini Dar es Salaam.


Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete (kulia) akijadiliana jambo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Andrea Pembe (kushoto) kwenye maafali hayo .

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi kuanza zoezi la kutunuku Shahada mbalimbali kwa wahitimu.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Andrea Pembe akizungumza kwenye Maafali hayo (PICHA ZOTE NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.

Wito umetolewa kwa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu nchini kuweka miundombinu itakayowawezesha wanafunzi wenye sifa wanaomaliza shahada za uzamili kuweza kujiendeleza kimasomo hadi kufikia shahada ya uzamivu (PhD) ili vyuo hivyo na Taasisi hizo kupata wataalamu wabobezi kwenye nyanja tofauti na kupunguza tatizo la upungufu wa wataalamu Vyuoni.

Wito huo umetolewa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) alipomuwakilisha Mkuu wa Chuo hicho Rais wa Awamu ya Pili Mzee Alli Hassan Mwinyi kwenye Mafali hayo.

Rais Kikwete amesema kuwa nchi yetu bado kuna idadi ndogo ya wahitimu wa Shahada za Uzamivu (PhD) tofauti na nchi jirani za afrika Mashariki ambapo vyuo vyao vinatoa idadi kubwa ya wahitimu wa Shahada ya Uzamivu na kufanya  kuwa na wataalamu wakutosha  wanaofundisha kwenye Vyuo vyao.

“Nchi yetu bado lipo tatizo la idadi ndogo ya wahitimu wa Shahada za uzamivu ukilinganisha na nchi jirani kama Kenya ambapo kwenye Maafali kama haya unakuta idadi kubwa ya wahitimu,nitoe rai kuweka mikakati ya kuwasaidia wanafunzi wenye uwezo kufikia hatua ya kupata PhD ili vyuo vyetu viweze kutumia waatalamu wake wa ndani” Amesema Rais Kikwete.

Aidha amewapongeza wahitimu wote na kuwataka wawe tayari kuitumikia nchi yao popote ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu inayowawezesha kufanyakazi zao kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa katika kutekeleza Majukumu yake Chuo hicho kimeendelea kuzingatia Sera na Mipango mikakati ya Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia pamoja na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto kwa lengo la kufanikisha malengo ya elimu ya juu na huduma za Afya nchini.

“Chuo kimezingatia vipaumbele vilivyoanishwa katika Sera ya elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa na ubora unaokidhi viwango na mahitaji ya soko la ajira Kitaifa, Kikanda, na Kimatafa” Ameeleza Dkt. Harrison Mwakyembe

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Andrea Pembe amesema kuwa Chuo hicho kimeendelea kutekeleza malengo na majukumu yake kupitia Skuli , Kurugenzi na Taasisi zake ambapo kwa mwaka wa masomo 2021/2022 Chuo hicho kimeweza kudahili wanafunzi 848 wa Shahada ya kwanza na wanafunzi 169 wa Stashahada katika fani mbalimbali za afya.

“Kwa mwaka huu wa masomo udahili wa masomo umeongezeka kwa asilimia nne (4%) ukilinganisha na udahili wa mwaka jana ambapo Chuo kilidahili wanafunzi 815 wa Shahada ya kwanza” Amesema Profesa Andrea Pembe.

Aidha amebainisha kuwa bado chuo hicho kinakabiliwa na changamoto kubwa ya udahili, katika mwaka wa masomo 2021/2022 kutokana na idadi kubwa ya walioomba kujiunga na chuo hicho kukosa nafasi ambapo kati ya wanafunzi 3297 wenye sifa za kujiunga na shahada ya kwanza ya udaktari wa binadamu ni wanafunzi 230 tu ndio walipata nafasi.

“Chuo bado kinaendeleza juhudi mbalimbali za kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kutosha katika Kampasi ya Mloganila na upatikanaji wa Rasilimali watu ya kutosha ili kuwezesha udahili wa idadi kubwa ya wanafunzi” Ameongeza Profesa Pembe.

Katika Mahafali hayo wahitimu wanne wamefanikiwa kupata Shahada ya juu ya Uzamivu ya udaktari wa Falsafa ambapo Naibu Mkuu wa Chuo hicho, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma aliwataja, Mourice Mbunde, Baraka Samweli, Mboka Jacob na Zuhura Idd Kimera ili kutunukiwa Shahada hiyo. 

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here