Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa ameyasema hayo mapema leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Wajasiriamali Wanawake kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, lililofanyika kwa lengo la kuenzi Siku ya Mwanamke Mjasiriamali Duniani.
“Naomba nitumie fursa hii kuwashauri na kuwasisitiza kuwa ni muhimu kurasimisha biashara zenu kwakuwa kuna manufaa makubwa utayapata kutokana na urasimishaji kuliko kufanya biashara katika hali zisizo rasmi,” alisisitiza Bw. Nyaisa.
Bw. Nyaisa ameainisha baadhi ya faida za urasimishaji biashara kuwa ni pamoja na biashara kutambuliwa na Serikali, wateja na jamii kwa ujumla, kuongeza fursa za kupata huduma za Serikali, kurahisisha upatikanaji wa mitaji kutoka serikalini na taasisi za kifedha kama vile mabenki na taasisi zinazotoa mikopo.
Amezitaja faida nyingine kuwa ni kupata huduma mbalimbali za Serikali kama vile, mafunzo, msaada wa kitaalamu na kiteknolojia.
Ameongeza kuwa endapo biashara itarasimishwa inaiwezesha Serikali kuboresha mipango yake ya kuwahudumia wajasiriamali na wafanyabiashara kwa kuwa inakuwa na uelewa wa idadi kamili ya wajasiriamali au wafanyabiashara waliopo.
“Urasimishaji biashara pia unasaidia kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwa walipa kodi wazuri na washiriki wenza wa Serikali katika kutoa huduma kwa jamii,”alifafanua Bw. Nyaisa
Aliongeza kuwa biashara inaporasimishwa inaongeza uaminifu kwa wateja kutokana na kutambulika na Serikali hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuingia mikataba ya kibiashara ama ubia na wafanyabiashara wengine pamoja na Makampuni ya ndani na nje ya nchi sambamba na kurahisisha upatikanaji wa dhamana kutoka Serikalini au taasisi binafsi.
Aidha Bw. Nyaisa amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wajasiriamali katika ujenzi wa uchumi endelevu, ukuaji wa biashara na kuongeza ajira kwa jamii ya Watanzania.
Kutokana na umuhimu wa wajasiriamali Bw. Nyaisa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya kisera, kisheria, kanuni, taratibu na mifumo ya utoaji huduma kwa kuzifanya kuwa wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha wakubwa na wadogo ili waweze kurasimisha biashara zao na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na urasimishaji huo.
“Wanawake wengi wamekuwa wakifanya biashara nyingi ndogondogo na nzuri na wamekuwa wakibuni nembo za biashara zao na kuzitumia kwa muda mrefu lakini ajabu ni kwamba hawazisajili , hali hii imepelekea baadhi ya watu kunakili majina ya biashara hizo na nembo na kuja BRELA kuchungulia kama zimesajiliwa na iwapo hazijasajiliwa basi wanasajili na kuzitumia , hali hii imesababisha wahusika kufikisha malalamiko BRELA,” amefafanua Bw.Nyaisa
Bw. Nyaisa aliongeza kuwa urasimishaji wa biashara unafanyika kwa kufanya sajili mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na Majina ya Biashara, Kampuni. Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Hataza, leseni za biashara na viwanda pamoja na usajili wa viwanda vidogo.
“Urasimishwaji huu unafanyika kwa njia ya mtandao ambapo kwa sasa mfanya biashara hahitaji kusafiri umbali mrefu kupata huduma, maboresho haya tuyatumie kama fursa kwa kuwa sasa sajili zote na utoaji Leseni unafanyika ndani ya muda mfupi sana,” amefafanua Bw. Nyaisa
Kongamano hilo lililoratibiwa na taasisi ya Youth Dreams Foundations limewakutanisha Wajasiriamali Wanawake wa Jiji la Dar es Salaam, ambao wamenufaika na mada mbalimbali zilizotolewa kuhusiana na ujasiriamali.
Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano BRELA