Home LOCAL WANANCHI NALASI MASHARIKI KUWASHIWA UMEME WA REA

WANANCHI NALASI MASHARIKI KUWASHIWA UMEME WA REA

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa tatu-kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (wa tatu-kulia) pamoja na Ujumbe waliofuatana nao wakati wa ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.

Kazi ya kuchimba mashimo kwa ajili ya kusimika nguzo za umeme ikiendelea katika kijiji cha Likuyu Mandela, wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, jana.

Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili wilayani Namtumbo (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini Wakili Julius Kalolo (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (kofia nyeusi), walipokuwa kwenye ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chilundundu Kusini, Adolphina Ndomba (wa kwanza-kushoto) na Kaimu Katibu Tarafa, Kata ya Nalasi Mashariki, Salumu Kijumu (wa pili-kushoto) wakizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (wa pili-kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa kwanza-kulia). Viongozi wa REA walikuwa katika ziara ya kazi wilayani Tunduru.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Ujumbe aliofuatana nao, wakiangalia uharibifu wa miundombinu ya umeme katika maeneo tofauti wilayani Tunduru na Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, walipokuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Nguzo zikiwa zimeharibiwa kwa kuchomwa moto katika maeneo tofauti wilayani Tunduru na Namtumbo, Mkoa wa Rukwa. Taswira hizi zilichukuliwa wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

Na: Veronica Simba, REA & nbsp; – TUNDURU.

Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, yuko katika hatua za mwisho kukamilisha upelekaji umeme katika kijiji hicho ili wananchi waunganishiwe na kuanza kunufaika na nishati hiyo.

Hayo yalibainika wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo aliyefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Tunduru, jana.

Wakizungumza na Uongozi wa Kata ya Nalasi Mashariki na wa Kijiji cha Chilundundu Kusini, viongozi hao wa REA walisema baada ya kufanya ukaguzi na kuzungumza na Mkandarasi, wamejiridhisha kuwa umeme utawashwa Nalasi ndani ya muda mfupi ujao.

Hivyo, waliwaomba viongozi wa Kata ya Nalasi kufikisha salamu zao kwa wananchi na kuwahamasisha kukamilisha maandalizi katika nyumba zao tayari kuupokea umeme.

Aidha, walimwagiza mwakilishi wa Mkandarasi ambaye ni muunganiko wa kampuni mbili za Guangdong Jianneng Electric Power Engineering Co. LTD na White City International Contractors LTD, kuhakikisha anakamilisha mapema iwezekanavyo, ujengaji wa miundombinu na kuwasha umeme ili kukidhi kiu ya muda mrefu ya wananchi wa Nalasi. 

Katika hatua nyingine, viongozi hao wa REA waliwaasa wananchi kutunza miundombinu ya umeme inayopita katika maeneo yao ili kuepusha hasara kubwa inayopatikana kwa serikali na wananchi wenyewe pindi kunapotokea uharibifu wake.

“Serikali inatumia fedha nyingi sana kufikisha miundombinu ya umeme vijijini ili kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo inapoharibiwa ni hasara kubwa siyo kwa serikali tu, bali pia na kwa wananchi wenyewe wa eneo husika,” alifafanua Mwenyekiti wa Bodi Wakili Kalolo.

Alisema kwamba yeyé pamoja na Ujumbe aliofuatana nao katika ziara hiyo wamesikitishwa kuona uharibifu wa miundombinu ya umeme katika maeneo kadhaa na kueleza kuwa hali hiyo inatokea katika maeneo tofauti tofauti nchini.</p><p>Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Saidy alisema uharibifu unaofanywa iwe ni kwa kudhamiria au kwa bahati mbaya unapaswa kuwekewa mikakati ya kuuzuia usiendelee kutokea ili kulinda miundombinu husika.

Akifafanua, alisema hilo linawezekana kwa viongozi katika maeneo mbalimbali kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa kushirikiana na kupeana taarifa.

Vilevile, Wakili Kalolo na Mhandisi Saidy waliwaelekeza viongozi wa Nalasi kuwatahadharisha wananchi kujiepusha na vishoka ambao wamekuwa wakiwatapeli wananchi katika maeneo mbalimbali ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa.

Walisema, Nalasi inaweza kukumbwa na wimbi hilo la vishoka kama ilivyo katika maeneo mengine yaliyofikiwa na umeme ambapo matapeli hao hutumia mwanya wa uhitaji mkubwa wa wananchi kuunganishiwa umeme kutekeleza vitendo vyao vya kitapeli.

“Wengi watakuja na kujitambulisha kwenu kama wafanyakazi wa REA na TANESCO, wapeni tahadhari wananchi ili wawe waangalifu,”alisisitiza Mhandisi Saidy

Aidha, waliwaelekeza viongozi wa Nalasi kuwakumbusha wananchi kuwa hivi sasa malipo yote ya serikali yanafanywa kupitia lipa namba hivyo wasikubali kulipa pesa taslimu kwa mtu yeyote na kupewa risiti.

Viongozi hao walitoa maelekezo kwa TANESCO ngazi ya Mkoa kufika Nalasi mara moja kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kujiandaa kuupokea umeme, kutunza miundombinu na kuepuka matapeli.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini na Mkurugenzi Mkuu wa REA wako katika ziara ya kazi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here