TIMU ya Tanzania (Taifa Stars) leo imekamilisha mechi zake za Kundi J kufuzu Kombe la Dunia kwa sare ya 1-1 na wenyeji, Madagascar jioni ya leo Uwanja wa Manispaaa ya Mahamasina Jijini Antananarivo.
Kikosi cha Taifa Stars kilitangulia kupata bao la mshambuliaji wa Simon Happygod Msuva dakika ya 24, kabla ya mshambuliaji wa Lierse K ya Ubelgiji, Hakim Djamel Abdallah kuisawazishia Madagascar dakika ya 74.
Wenyeji, Madagascar walimaliza pungufu baada ya beki wa Saint-Pierroise ya Réunion, Pascal Razakanantenaina kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 83 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano baada ya kumchezea rafu Msuva nje kidogo ya boksi.
Mechi nyingine ya Kundi J leo, wenyeji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Benin Uwanja wa Martyrs de la Pentecôte Jijini Kinshasa.
Kwa matokeo hayo, DRC inamaliza kileleni kwa pointi zake 11, ikifuatiwa na Benin 10 na Taifa Stars nane, wakati Madagascar imeshika mkia kwa pointi zake nne.
Kongo inakwenda hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Qatar ambako itakutana na mmoja wa washindi wa makundi mengine tisa katika mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atakuwa mmoja kati ya wawakilishi watano wa Afrika Kombe la Dunia mwakani.