Na: Lilian Lundo – MAELEZO.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi Agosti 2022, ambapo imeelezwa kuwa, sensa hiyo itafanyika kidigitali kwa asilimia mia kwa nchi nzima.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa, amesema hayo leo Novemba 17, 2021, Jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya kompyuta kutoka Serikali ya Uingereza.
“Tanzania inatarajia kufanya sensa ya Sita Agosti, 2022, sensa hiyo tutaifanya kidigitali kwa asilimia mia ili kurahisisha zoezi la kuhesabu watu na makazi. Tumeshafanya majaribio kama ambavyo Umoja wa Mataifa unavyotuelekeza kufanya,” alisema Dkt. Chuwa.
Ameendelea kusema kuwa, maandalizi ya sensa hiyo yamefikia asilimia 50, ambapo kwa sasa wanaendelea na zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabu watu pamoja na kuhamasisha watu kujitokeza kushiriki katika zoezi hilo la kuhesabiwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini, Rob Swinkels, amesema kuwa, wametoa compyuta hizo kwa Ofisi ya Takwimu Bara na Zanzibar ili kuboresha zoezi la sensa na kupata data sahihi, pia kurahisisha zoezi la ukusanyaji data kwa haraka ili Serikali na Taasisi nyingine ziweze kufanyia kazi data hizo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Jacqueline Mahon amesema kuwa, wametoa kompyuta hizo ili kuhakikisha kila Mtanzania anahesabiwa ili kupata takwimu ambazo ni sahihi katika sensa hiyo itakayofanyika Agosti, 2022.
Aidha, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Anne Makinda amesema kuwa, kompyuta hizo sio msaada sababu data zitakazopatikana hazitatumika Tanzania peke yake bali zitahitajika pia katika takwimu za dunia na hata mashirika ya kimataifa kama vile UNFPA na Benki ya Dunia.
Serikali ya Uingereza imetoa kompyuta mpakato 28 na kompyuta za mezani 20 ambazo zitatumika katika sensa ya watu na makazi Agosti, 2022 hapa nchini.