Na: Mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo, ametembelea kambi na mazoezi ya Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu, Tembo Warriors, wanaoendelea na maandalizi ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika (Canaf) inayofanyika Dar es Salaam, Tanzania.
Katika matembezi hayo waziri alikuwa ameambatana na Mawaziri wa Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Jenister Mhagama, Katibu Mkuu wa Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu-Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda, na viongozi wengine wa Serikali, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa salaam za Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na motisha ya Rais kwa timu hiyo.
“Mhe Rais anafahamu mko hapa mnajiandaa kuipigania nchi na amesema nije hapa kwa niaba yake na ametoa kiasi cha Shilingi milioni 150 kuhakikisha ninyi na timu zote za Afrika zinazokuja Tanzania zinakaa hapa vizuri,” alisema Mhe. Majaliwa.
Tanzania ni mwenyeji wa mashindano hayo ambapo timu kutoka nchi 15 zinashiriki kwa ukanda wa Afrika ambapo timu nne zitafuzu kwenda mashindano ya dunia.