Home BUSINESS PROF. MKUMBO: WIZARA IMEKUSUDIA KULETA MABADILIKO YA KISERA, KIMUUNDO NA KIMAJUKUMU

PROF. MKUMBO: WIZARA IMEKUSUDIA KULETA MABADILIKO YA KISERA, KIMUUNDO NA KIMAJUKUMU




DODOMA

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Wizara imekusudia kuleta mabadiliko makubwa ya Kisera, Kimuundo na kimajukumu kwa taasisi zake ili kutekeleza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi shindani unaoongozwa na Viwanda.

Prof. Mkumbo ameeleza hayo Novemba 06, 2021 alipokuwa akifungua na kuongoza kikao kazi cha siku mbili cha Menejimenti, Taasisi zote na Wenyeviti wa Bodi wa  Taasisi zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kilichofanyika Ukumbi wa Zimamoto Dodoma.

“Tumefanya mapitio ya Taasisi zetu za TIRDO,TEMDO, CAMARTEC na SIDO na kuna mapendekezo makubwa yatakayofanya kutoka zilipo sasa na zinaendelea mbele na nimekusudia kufanya mapitio ya kimuundo na kimajukumu kuhusu mashirika ya TBS na WMA vilevile Taasisi za NDC na EPZA” ameeleza Prof. Mkumbo.

Prof. Mkumbo ameeleza kuwa wamekusudia kufanya mapitio ya Sera na utungaji wa sera mpya za sekta ya Viwanda na Biashara hasa Sera mbili mama  Sera ya Maendeleo ya Viwanda vidogo na Biashara ndogo na Sera ya biashara nyingine.

Aidha, Prof. Mkumbo amebainisha kuwa katika kikao hicho watapata mawasilisho ya Wizara na Taasisi kwa yale wanayoyafanya na waliyoyafanya ikihusisha mambo ya kimkakati ndani ya taasisi zote na kukumbushana majukumu ya msingi yakiwepo majukumu makuu mawili ya kuwezesha biashara katika nchi na kuwezesha maendeleo ya viwanda.

Vilevile, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kupitia Idara ya Sera na Mipango, Wizara imepanga kutengeneza mkataba wa utendaji kazi ili kupima mafanikio ya Wizara na Taasisi zake na kuboresha ufanisi wa kuwahudia wateja.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here