Home LOCAL HOSPITALI YA WILAYA TUNDURU NA MDH WATUMIA MOBILE CLINIC KUIBUA WAGONJWA WA...

HOSPITALI YA WILAYA TUNDURU NA MDH WATUMIA MOBILE CLINIC KUIBUA WAGONJWA WA KIFUA KIKUU

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtonya Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa wataalam wa kitengo cha kifua kikuu Hospitali ya wilaya Tunduru na wataalam wa Shirika lisilo la Kiserikali ya MDH inayotolewa kwa kutumia vifaa mbalimbali kwenye gari maalum(Mobile Clinic)ambayo imerahisisha kuwafikia wananchi wengi hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni.

Na: Muhidin Amri,Tunduru

SERIKALI kupitia Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na shirika lisilo la Serikali la MDH,imeanza kampeni ya kuwapima wananchi wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia gari maalum lenye vifaa tiba  mbalimbali(Mobile Clinic).

Kampeni hiyo inatajwa  yenye mafanikio makubwa kwani imerahisisha  utendaji kazi kwa wataalam wa kitengo cha kifua kikuu kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa watu wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo.

Aidha, katika kampeni hiyo watu wanaofanyiwa uchunguzi wanapewa majibu ya papo hapo na kuanzishiwa dawa wote wanaobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, jambo lililowavutia wananchi wengi kujitokeza  kupata matibabu ya kifua kikuu na kuokoa muda wa wananchi wanaofika kupata huduma ya uchunguzi.

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, hali ya maambukizi ya kifua kikuu katika wilaya hiyo ni kubwa  na hali hiyo inasababishwa na changamoto ya jiografia ya wilaya hiyo kwa baadhi ya maeneo  kutofikika kwa urahisi.

Alisema, kuna maeneo mengine huduma za afya zinapatikana mbali na maeneo mengine hakuna kabisa huduma za matibabu hivyo wananchi kukosa tiba sahihi  badala yake wanaamua kukimbilia  kutumia tiba asili na tiba mbadala.

Alisema,huduma tembezi(mobile clinic)ni msaada mkubwa katika wilaya ya Tunduru kwani tangu walipoanza kutumia huduma hiyo wamefanikiwa kufika maeneo mengi ya pembezoni na wananchi wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu.

Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa mkoa wa Ruvuma Dkt Xavier Mbawala alisema,lengo la kutumia gari hilo ni moja ya jitihada za Serikali ya kuwafikishia wananchi huduma pale wanapoishi.

Alisema, wananchi wengi  hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni wanashindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma kutokana na changamoto mbalimbali, kwa hiyo kupatikana  kwa gari hilo kutasaidia wananchi kufikiwa na huduma ya uchunguzi na tiba sahihi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Dkt Mbawala alisema, kampeni hiyo itafanyika katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma na kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi pindi gari na wataalam wa kitengo cha kifua kikuu wanapofika katika maeneo yao.

Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Mtonya,wameishukuru Serikali  kwa kuwafikishia huduma  hiyo karibu na makazi yao kwa sababu imewapunguzia gharama kubwa kufuata  huduma ya kupima kifua kikuu.

Bakari Siwili mkazi wa kijiji cha Mtonya alisema, changamoto kubwa kwa wananchi walio wengi hasa wanaoishi vijijini ni umbali kutoka katika maeneo yao kwenda Hospitali ya wilaya Tunduru mjini.

Alisema, kuna wananchi wamepoteza maisha kwa kukosa tiba sahihi ya ugonjwa huo na wengine wako majumbani licha ya matibabu ya kifua kikuu kutolewa bure.

Hata hivyo alisema, baadhi ya wananchi hususani wanaoishi vijiji vya pembezoni wanashindwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za matibabu kutokana na kushindwa kumudu gharama za usafiri.

Hadija Faki alisema, uwepo wa gari hilo limesaidia kuwafikia wananchi wengi wanaoishi maeneo ya pembezoni  kwa ajili ya uchunguzi na kupata tiba.
MWISHO.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here