Home LOCAL MAJALIWA: SERIKALI INATAMBUA MCHANGO UNAOTOLEWA NA TAASISI ZA KIDINI NCHINI

MAJALIWA: SERIKALI INATAMBUA MCHANGO UNAOTOLEWA NA TAASISI ZA KIDINI NCHINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislam ya Isitqaama, Sheikh Seif Ally Seif (wa pili kulia) kukagua maeneo mbalimbali ya Msikiti wa Jamiu Assaliheen wa Ikwiriri wilayani Rufiji baada ya kuufungua, Oktoba 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Baadhi ya Waislam wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua msikiti wa Jamiu Assaliheen wa Ikwiriri wilayani Rufiji, Oktoba 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua msikiti wa Jamiu Assaliheen wa Ikwiriri wilayani Rufiji, Oktoba 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipofungua msikiti wa Jamiu Assaliheen wa Ikwiriri wilayani Rufiji, Oktoba 1, 2021. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislam ya Isitqaama, Sheikh Seif Ally Seif, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Juumiya hiyo, Sheikh Badar bin Sood na kulia ni Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua msikiti wa Jamiu Assaliheen wa Ikwiriri wilayani Rufiji, Oktoba 1, 2021. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Kiislam ya Isitqaama, Sheikh Badar bin Sood , Mwenyekiti wa Juumiya hiyo, Sheikh Seif Ally Seif na kulia ni Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaheshimu, inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini katika kujenga jamii ya wacha Mungu, wenye kutii mamlaka na sheria.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za kidini kujiepushe kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa na badala yake ziendelee kushirikiana na Serikali katika kujenga Taifa la watu wenye hofu ya Mungu, heshima, upendo na wenye kudumisha amani na utulivu nchini.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba Mosi, 2021) kwenye hafla ya uzinduzi wa msikiti wa Jamiu Assaliheen uliojengwa na taasisi ya Istiqaama katika Kata ya Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.  Msikiti huo una uwezo wa kutumiwa na waumini 500 kwa wakati mmoja na una vyumba vinne vya madrasa kwa ajili ya kutoa elimu ya dini na malezi mema.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na taasisi zote za kidini zenye nia safi na thabiti ili kuhakikisha miradi na mipango mbalimbali ya kijamii na kiroho yenye manufaa kwa umma wa Watanzania inaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.

“Sote ni mashahidi kuhusu mchango mkubwa unaotolewa na madhehebu au taasisi za kidini katika jamii yetu. Taasisi za kidini nchini zimekuwa zikijihusisha kwa kiwango kikubwa na utoaji wa huduma za kijamii hususan elimu, maji, afya, kusaidia watu wenye uhitaji kama vile yatima na wajane sambamba na malezi na utoaji wa huduma za kiroho.“

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya ya Istiqaama kwa kazi nzuri wanazozifanya nchini ikiwemo ya kujenga mshikamano baina ya waislamu wa madhehebu mbalimbali lakini pia baina ya waislamu na waumini wa dini nyingine . “Hivyo basi, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie sote moyo wa subra na kujitolea katika mambo ya heri.“

“Aidha niwapongeze kwa kazi nzuri ya kujenga misingi mizuri ya kiroho na kimaadili kwa vijana wetu ambao ndiyo Taifa na viongozi wetu wa kesho. Jambo hili ni la msingi sana kwani ni dhahiri kuwa hakuna Taifa lolote duniani linaloweza kufanikiwa bila ya kuwa na misingi imara ya kiroho na kimaadili.“

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania Sheikh Badar bin Sood amempongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendeleza umoja, amani, mshikamano na maendeleo kwenye kila nyanja kwa Watanzania wote.

Naye, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally amewakumbusha waumini wa dini ya kiislam na watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchanja chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19 ili kuongeza kinga na kujilinda na ugonjwa huo.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkuu wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania Sheikh Khalifa, Sheikh, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif, Naibu Balozi wa Oman nchini, Dkt. Salim Al Harbin, Mwakilishi wa Mufti wa Oman, Sheikh Dr Wail Al Harasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here