Home BUSINESS GST YAGUNDUA UWEPO WA MADINI YA DHAHABU LUMBANGA WILAYANI MALINYI

GST YAGUNDUA UWEPO WA MADINI YA DHAHABU LUMBANGA WILAYANI MALINYI

 

Na. Tito Mselem.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele ametoa wito kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kuitangaza Wilaya ya Malinyi baada ya kugundulika kuwa na uwepo wa madini ya dhahabu ili kuwavutia wawekezaji wilayani humo.

Akizungumza katika kikao cha kupokea mrejesho wa utafiti uliofanywa na GST wilayani Malinyi, Masele amesema kuwa, wilaya yake sasa imeingia kwenye ramani ya kuwa na madini ya dhahabu hivyo amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuitumia fursa ya uwepo wa madini hayo ili kubadili maisha yao kuwa bora zaidi.

“Naomba nitumie fursa hii kuonesha furaha yangu ya hali ya juu baada ya wenzetu wa GST kututhibitishia kwamba wilaya yetu ya Malinyi ina madini aina ya dhahabu hivyo nitoe wito kwa wananchi wa Malinyi muitumie fursa hii muhimu kuhakikisha inawanufaisha watu wa Malinyi na taifa letu kwa ujumla,” amesema Masele.

Aidha, Masele amewashukuru wataalamu wa GST kwa kufanya utafiti wilayani humo na kuleta mrejesho wa utafiti walioufanya ambapo amesema uwepo wa madini wilayani humo utasaidia kufungua fursa nyingine ikiwemo kukuwa kwa uchumi wa kilimo na biashara mbalimbali zinazofanyika wilayani humo.

Pia, Masele ametoa wito kwa Tume ya Madini kuhakikisha wanafungua soko la madini na kuleta wataalamu wa madini ili waweze kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini na kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Jioloji Maswi Solomon Mwita amesema, GST imefanya utafiti wilayani Malinyi na kugundua uwepo wa madini ya dhahabu ambayo ni fursa kwa wawekezaji kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina. 

Mwita amesema GST ndiyo Taasisi inayojishughulisha na tafiti mbalimbali za jiosayansi ikiwemo madini na kuishauri Serikali na wadau wengine wa Sekta ya Madini namna bora ya kuendeleza rasilimali madini. Hivyo, ameishauri Serikali ya wilaya ya Malinyi kwa kushirikiana na GST na STAMICO kuendelea kufanya utafiti zaidi baada ya utafiti wa awali kugundua uwepo wa madini katika eneo la Lumbanga wilayani humo.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi-GST, Zortosy Mpangile Maganga amesema kuwa mwishoni mwa mwaka 2020 timu ya wataalamu kutoka GST ilifanya utafiti wa jiolojia katika eneo la Lumbanga wilayani Malinyi ambapo walichukua sampuli za miamba na kupelekwa katika maabara ya GST yenye ITHIBATI ya kimataifa kwa ajili ya uchunguzi wa madini ya dhahabu lakini pia kwa ajili ya utambuzi wa aina ya miamba iliyopo eneo hilo.

Mpangile amesema, utafiti wa maabara ulibaini uwepo wa madini ya dhahabu yenye kiwango cha 4.1 gramu kwa tani moja katika eneo la Lumbanga. Aidha, matokeo ya utafiti wa jiofizikia yameonesha mipasuko katika miamba yenye uelekeo tofauti tofauti.

Sambamba la hilo Mpangile amesema, dhumuni la utafiti huo ilikuwa ni kukusanya taarifa kwa ajili kutengeneza ramani za jiolojia na jiofizikia katika maeneo ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kuwasaidia kuanisha miamba ya madini pamoja na uelekeo wake katika eneo la Lumbanga. 

Kutokana na utafiti wa jiolojia, jiofizikia na uchunguzi wa maabara, GST inapendekeza ufanyike utafiti wa kina ili kugundua uwingi wa mashapo katika eneo hilo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here