Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara na Mazingira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ndanda (CCM) Mhe.Cecil Mwambe akichagia mada wakati wa Semina ya utekelezaji wa mfumo wa Stakabadhi za ghala kwa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara na Mazingira,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakati wa Semina iliyofanyika bungeni Jijini Dodoma.
Mumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA Mhe.Kunti Majala,akichagia mada wakati wa Semina ya utekelezaji wa mfumo wa Stakabadhi za ghala kwa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara na Mazingira,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakati wa Semina iliyofanyika bungeni Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna, Fullshangwe Blog Dodoma
WIZARA ya Viwanda na Biashara imeahidi kufanya maboresho ya kero zinazojitokeza kwenye Mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwamo ni pamoja na kufanya mapitio kwenye sheria na kanuni ili uwe na tija kwa wakulima nchini.
Hayo yameelezwa jana Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara hiyo , Exaud Kigahe wakati akizungumza katika semina iliyotolewa na Wizara hiyo kwa Wabunge kutoka Kamati tano za Bunge kuhusu utekelezaji wa mfumo huo.
Kamati hizo ni Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda , Biashara na Mazingira, Kamati ya Kilimo,Mifugo na Maji, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa ,Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali.
Akizungumza kwenye semina hiyo, Kigahe amesema Serikali ina mikakati ya kutatua changamoto ambazo zimejitokeza katika kutekeleza mfumo huo ikiwa ni pamoja na kuboresha kujenga maghala mengi ili kupunguza changamoto za wakulima wadogo kupeleka maghala ya umbali.
“Serikali inaendelea kusajili maghala na kukaribisha wadau kujenga kwa kuwa ni biashara nzuri ili kusaidia kuhifadhi mazao na kuuza kwa bei nzuri,”amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha,Naibu Waziri Kigahe amesema wameweka wakaguzi ili kudhibiti ujanja ujanja unaofanywa wa kuwapunja wakulima pamoja na kukagua ubora kabla ya kuhifadhi ghalani kama Mbunge Kunti Majala alivyoshauri kukagua ubora ili kuhakikisha bidhaa unayolipwa iwe halali na haijachanganywa na vitu.
Pia,ametoa wito kwa Wabunge wa Kanda ya Ziwa kuanza kutoa elimu kwa wananchi kulima kilimo biashara kwa kuwa mazao ya choroko na dengu yana soko na kuahidi serikali itatoa elimu kwa kanda hiyo.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, amesema Mfumo huo una manufaa mbalimbali ikiwemo wakulima kupigania bei nzuri katika soko kwa kuhamasisha kutumia mfumo wa pamoja kukusanya na kuuza, kutoa uhakika wa ubora na bidhaa na Mfumo wa uthibitisho, kupunguza mashaka na gharama za ushughulikiaji kwa wafanyabiashara wa bidhaa na wakulima wakati wa kufanya biashara,
Amesema dhumuni la kuanzishwa mfumo huo ni kukuza juhudi za serikali kurasimisha mifumo ya masoko iliyopo ili kupunguza vipingamizi mbalimbali vinavyokwaza uzalishaji wenye tija.
“Mfumo huo umesaidia kuweka utaratibu wa kupata taarifa na takwimu za soko na mauzo za kuaminika kwa wadau mbalimbali, kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wa bidhaa wenyeji katika biashara ya kimataifa, kuhimiza usindikaji nchini wa mazao ya msingi kwa lengo la kuongeza thamani nakukuza uendelezaji wa viwanda,”amesema.
Mrajisi Mkuu wa Tume ya Vyama vya ushirika Tanzania, Dk. Benson Ndiege amesema mfumo huo ukiimarishwa utakuwa mkombozi wa mkulima na kwamba Tume hiyo imeshaanza mchakato wa kukusanya maoni na kurekebisha Sheria ya Ushirika