Home BUSINESS WAFANYABIASHA RUKWA LIPENI KODI KWA WAKATI- RC MKIRIKITI

WAFANYABIASHA RUKWA LIPENI KODI KWA WAKATI- RC MKIRIKITI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti (kulia) akiwa na Afisa Habari toka Mamlaka ya Mapato Tanzania Rachel Mkundai (kushoto) jana wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Sumbawanga kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania Richard Kayombo akizungumza kwenye semina na wafanyabiashara mjini Sumbawanga jana.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ( wa tano toka kulia) akiwa na wafanyabiashara wa Rukwa mara baada ya kufungua semina ya umuhimu wa ulipaji kodi wa jana Sumbawanga.

(Habari na picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)
Na: Amani Kassimba, RUKWA.

Wafanyabiashara wa mkoa wa Rukwa wametakiwa kuwa na mtindo wa kulipa kodi kwa hiari ili kuwezesha serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti jana (13.09.2021) wakati alipofungua semina ya utoaji elimu ya kodi iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Sumbawanga.

“Ni vizuri wafanyabiashara wote mkawa na utaratibu wa kulipa kodi kwa hiari badala ya kusubiri mivutano kwani serikali inategemea fedha hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa umma” alisema Mkirikiti.

Katika semina hiyo iliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali wa mjini Sumbawanga, Mkirikiti aliwataka watumie pia fursa ya fedha zinazotolewa na serikali kwa miradi ya afya, shule na miundombinu ili washiriki  ujenzi wa miradi hiyo.

Mkirikiti aliongeza kusema serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuleta fedha nyingi za miradi ikiwamo Shilingi Milioni 750 za hii karibuni zilizotokana na tozo ya miamala ambazo zinakwenda kujenga vituo vitatu vya afya kwenye tarafa za mkoa wa Rukwa.

Mkuu huyo wa Mkoa alitaja vituo vya afya vitakavyojengwa kuwa ni  Mwazye ( Kalambo), Kate ( Nkasi) na Kipeta ( Sumbawanga) ambapo kila kimoja kimepatiwa Shilingi Milioni 250 kwa awamu ya kwanza mwezi Agosti mwaka huu.

“Ninapenda wafanyabiashara wa Rukwa muwe na taarifa za miradi na fedha zinazotolewa na serikali ili iwe chachu kwenu kujitokeza kutekeleza na kutoa huduma ili mpate fedha pia serikali ipate kodi badala ya kuachia miradi hiyo wafanyabiashara toka nje ya Rukwa” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania Richard Kayombo alisema wapo mkoani Rukwa  kuelimisha walipa kodi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na kusikiliza changamoto zao.

Kayombo aliongeza kusema TRA itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato bila mikwaruzano ambapo msingi mkubwa ni kutekeleza Agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuona kodi inakusanywa kwenye mazingira rafiki sio kutumia nguvu.

Naye Anusisye Thomas mkandarasi wa ujenzi alitoa ombi kwa serikali ya mkoa kuwezesha wazabuni na wakandarasi wa ndani kupata kazi za miradi ya serikali ili wanufaike kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya mkoa wa Rukwa badala ya kutumia wakandarasi wa nje.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Afisa Habari Mkuu,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

SUMBAWANGA

14.09.2021

 


Previous articleKAMATI YA SERA YA FEDHA BOT YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA SERA HIYO KWA KIPINDI CHA MWEZI JULAI NA AGOSTI 2021
Next articleKIUNGO WA SIMBA QUEEN ACHAGULIWA KIKOSI BORA CECAFA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here