Home LOCAL RC SENYAMULE: TUFANYE MAPINDUZI YA KIUCHUMI.

RC SENYAMULE: TUFANYE MAPINDUZI YA KIUCHUMI.

 

Anaripoti, Paul Zahoro: RS GEITA.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuwa na mipango thabiti ya kutumia Kilimo, Uvuvi na Ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija kwenye uzalishaji ili kuongeza mapato ya Halmashauri hatimaye kuwainua wananchi kiuchumi.

Akizungumza leo septemba 03, 2021 kwenye kikao cha Kimkakati kilichoketi mahsusi kujadili namna bora ya kuinua Mkoa kwenye mapato kuendana na uboreshaji wa huduma kwa jamii ambapo kimewakutanisha viongozi wa Wilaya na Halmashauri za Mkoa wa Geita, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa siku 90 kwa viongozi hao kurudi na mpango wa kusaidia wananchi.

“Tufanye Mapinduzi ya Kiuchumi, zipo fursa za Kilimo, Uvuvi, Mifugo ambazo hazijafanyiwa kazi ipasavyo sasa twendeni tukaweke mikakati ya pamoja ya kufanya Mapinduzi ya Kiuchumi.” Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa viongozi hao kusimamia taratibu za kutoza ushuru na tozo kwenye Shughuli za Uchimbaji Madini ili mapato ya ndani kutokana na Shughuli hizo yasiwe kandamizi na tozo ziende kwenye uboreshaji wa Miundombinu ya Shughuli husika ili ziwanufaishe walio kwenye sekta hiyo.

Mhe. Senyamule ameshukuru Rais Samia Suluhu kwa nia ya dhati ya kuinua sekta ya Elimu nchini ambapo siku za karibuni Mkoa wa Geita umepokea fedha za kujenga zaidi ya  madarasa 1400 na amewaagiza Wakurugenzi kuratinu na kusimamia kwa umakini mkubwa ili Miradi hiyo iishe kwa wakati na ubora unaokusudiwa.

Hata hivyo Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa viongozi hao kuwa na mkakati wa kumaliza changamoto ya madarasa na vyumba vya madarasa kwa kutumia vyanzo vya ndani pasipo kusubiri fedha kutoka serikali kuu kwani tatizo la Msongamano wa wanafunzi bado ni kubwa Mkoani Geita.

Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewapongeza viongozi hao kwa juhudi kubwa zilizopelekea   kuwa na 92% ya uwepo wa vituo vya kutolea huduma za Afya na ameagiza idara hiyo kupeleka Watumishi kwenye Zahanati mpya 32 mpya zilizokamilika ili ziweze kutoa huduma kwa wananchi na kukamilisha Miundombinu ya Zahanati 105 zilizo kwenye hatua mbalimbali ya ujenzi.

Akiwasainisha Wakuu wa Wilaya Mikataba mipya ya Miaka Mitano ya Utendaji kazi na Usimamizi wa Shughuli za Lishe, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka Maafisa Lishe kwenye Halmashauri zote kusimamia vema Shughuli za Lishe kama wanavyosimamia programu zingine za serikali ili kufikia lengo la Taifa la kuiokoa jamii kutoka kwenye udumavu unaofifisha juhudi za ukuaji wa Uchumi.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amesisitiza ukusanyaji wa Mapato kufuata Sheria na taratibu za fedha ikiwa ni pamoja na matumizi ya Vifaa maalumu vya kukusanyia mapato (POS) na sio vinginevyo ili kuzuia upotevu wa Mapato.

Hata hivyo ,Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji akawaagiza kutatua kero za wananchi kwa wakati ili kuisaidia jamii kwani hoja nyingi ni za kawaida na wanahitaji msaada wa haraka.

Baada ya wito wa kufuata taratibu zinazoshauriwa na wataalamu wa Afya katika kupambana dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 ikiwa ni pamoja na Chanjo ya Ugonjwa huo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa Viongozi kuendelea na maandalizi ya Shughuli ya Kitaifa ya Kukimbiza na Kuzima Mwenge Maalumu wa Uhuru 2021 inayotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba pamoja na Maonesho ya Nne ya Teknolojia ya Madini na uwekezaji yatakayifanyika kuanzia Septemba 16-26.

Awali, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji, Ndugu James Chiragi alitoa wito kwa Halamshauri kuhakikisha 20% ya mapato yatokanayo na Kilimo, 15% kutoka kwenye Mifugo na 5% kutoka wenye Uvuvi zirejeshwe kwenye sekta hizo kama Sheria unavyosema ili kuboresha Shughuli za Ugani.

“Unapoongeza thamani kwenye mazao ya Uvuvi, unaongeza mnyororo wa biashara ambapo wananchi wengi watahusika na mwisho tija kwenye zao hilo itaongezeka”.  Tito Mlelwa, Afisa Uvuvi wa Mkoa.

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa, Ndugu Daniel Mapunda amebainisha kuwa zuio la kusafisha Kaboni nje ya Mkoa limekua na faida sana kwenye ukuaji wa sekta hiyo kwani limepelekea ongezeko la ‘Elution’  kufikia 40 kutoka 15 za siku za nyuma Mkoani Geita.

Akiwasilisha mada, Afisa Elimu Mkoa Anthony Mtweve amefafanua kuwa zaidi ya vyumba vya madarasa elfu 11 vitahitajika ifikapo mweka 2022 ili kukabiliana matatizo la Msongamano wa wanafunzi kwenye madarasa na kwamba kwa sasa madarasa 8830 yanahitajika.

.

Previous articleTCU YATOA MWENENDO WA UDAHILI WA SHAHADA YA KWANZA KWA MWAKA WA MASOMO 2021/2022
Next articleTANZANIA ITAPATA FAIDA NYINGI IKIRIDHIA MKATABA WA AfCFTA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here