Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule Septemba 11, 2021 amefanya ufunguzi wa Shule ya Sekondari ya binafsi ya Royal Family iliyopo Mtaa wa Magogo iliyogharimu zaidi ya Milioni 700 ambapo mwaka 2022 inatarajiwa kuanza rasmi kwa kidato cha kwanza kwani Miundombinu kama vyumba vya madarasa 12, Maabara za sayansi, Ofisi za Walimu, mabweni na bwalo la chakula vimeshajengwa.
Akizungumza kwenye Hafla ya kuwaaga wanafunzi wa Darasa la Saba iliyoambatana na hafla ya uzinduzi wa Shule ya Sekondari ya Royal Family, Mhe. Senyamule amempongeza Mkurugenzi wa shule hiyo kwa kuchangia kwa kiwango kikubwa kuufanya mkoa wa Geita kushika nafasi nzuri kitaifa katika mitihani ya darasa la saba kutokana na Uongozi thabiti na umahiri wa Walimu.“Kwakweli niseme tu wazi kwamba shule za Royal Family mnawaandaa vizuri watoto kitaaluma na ndio maana tumeshuhudia vipaji vikubwa hapa, hongereni sana Walimu kwa maandalizi mazuri kwa watoto hawa na Mungu awabariki sana”, amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa.
Akiwa na uso wa bashasha Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan siku za hivi karibuni ameleta Fedha Tshs. Bilioni 27 kwenye sekta ya Elimu na kwamba fedha hizo zitajenga zaidi ya vyumba vya madarasa elfu moja Mkoani Geita na kuondoa kero ya Msongamano wa wanafunzi madarasani.
Vilevile, amesema kuwa shule ya Msingi Royal Family imekuwa inafanya vizuri katika Matokeo ya darasa la Saba kitaifa kuanzia mwaka 2017 ambapo imekuwa inashika nafasi ya kwa kwanza Kimkoa na imedumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu na kwamba jambo hilo linachangia Mkoa kushika nafasi nzuri kitaifa wakati wa kukokotoa wastani wa jumla kwa mikoa yote nchini.Mhe. Senyamule aliendelea kuimwagia sifa shule hiyo ambapo ameongeza kuwa shule nyingi zimekuwa zinashika nafasi ya kwanza Mara moja tu na kupromoka hadi nafasi ya pili na kuendelea lakini kwa shule ya msingi Royal family ni tofauti kwasababu imeweza kuhimili kudumu kwenye nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Mhandisi Lazaro Philipo, Mkurugenzi wa Shule za Royal Family ametumia wasaa huo kuwakaribisha Wazazi kuleta wanafunzi kwenye shule Mpya ya Sekondari Royal Family itakayoanza mwezi januari 2022 na amebainisha kuwa shule hiyo yenye mabweni yenye uwezo wa kubeba zaidi ya wanafunzi 120 na itafanya Mapinduzi makubwa kwenye Elimu Mkoani hapa.“Tumeitikia wito wa Serikali kwa kaulimbiu ya Serikali ya viwanda yenye shabaha ya kufikia Uchumi wa Kati wa juu ifikapo mwaka 2025 na ndio maana tunajikita kwenye kuelimisha jamii hasa masomo ya sayansi.” Amesisitiza Mhandisi Philipo.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Deogratias Katunzi amemuomba mkuu wa mkoa wa Geita Rosemary Senyamule kusaidia kutengenezwa kipande cha Barabara inayoelekea kwenye shule hiyo ambacho amesema kinakadiliwa kuwa na urefu wa mita sabini ambapo Mhe. Mkuu wa mkoa ameahidi kupeleka watalaamu kutoka wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kwenda kufanya tathimini ya barabara hiyo na kutoa ushauri wa kitaalumu na watalifanyia kazi baada ya ushauri huo.