Home BUSINESS MKUU WA WILAYA YA GEITA WILSON SHIMO AIOMBA NHC KUJENGA NYUMBA GEITA

MKUU WA WILAYA YA GEITA WILSON SHIMO AIOMBA NHC KUJENGA NYUMBA GEITA

Ofisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Domina Rwemanyila akitoa maelezo kwa wageni waliopita kwenye banda lao ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo (wa kwanza kulia mwenye shati nyeupe),  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Zahra Michuzi (katikati) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Wanga (wa tatu kulia) kuona shughuli za Shirika hilo kwenye maonesho ya nne ya Sekta ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Mjini Geita.

Na: Domina Rwemanyila GEITA.

MKUU wa Wilaya ya Geita Wilson Shimo ameliomba Shirika la Taifa – NHC kujenga nyumba za makazi katika Wilaya hiyo kutokana na uhitaji wa nyumba Wilayani humo.

Shimo amesema kuwa ushiriki wa NHC katika Maonesho hayo yalete faraja kwa wakazi wa eneo hili kwa kujenga nyumba za makazi kwani uhitaji ni mkubwa mno na NHC inaweza ikapunguza adha ya upatikanaji wa nyumba Wilayani humo.

Ameyasema hayo leo (tarehe 20/09/2021) wakati alipolitembelea banda la NHC akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Zahra Michuzi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Wanga katika Maonesho ya nne ya Teknolojia ya Uwekezaji Sekta ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili – EPZ Mkoani Geita.

“Tunafahamu kuwa NHC tayari mlikwishajenga nyumba hamsini katika eneo hili la Bombambili lakini nyumba hizi ziliuzwa na zingine kupangishwa lakini bado tunatamani sana mje mtujengee nyumba zingine ambazo nina uhakika hata kabla mradi haujakwisha tayari nyumba zote zitakuwa zimekwisha, hivyo basi niwaombe mje kuwekeza bado hamjachelewa” Amesema Shimo.

Ameongeza kusema kuwa Shirika la Nyumba la Taifa limejenga miradi mbalimbali nchini ambayo kupitia miradi hiyo limeweza kuwekeza kwa kiasi kikubwa, hivyo basi sasa ni wakati wa kuwekeza tena Geita kwa ujenzi wa nyumba za makazi ambazo kwa Wilaya ya Geita zitawasaidia wananchi wenye uhitaji ambao ni wengi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita John Wanga amesema Geita ni mkoa wenye wageni wengi, mbali ya wakazi wa eneo hili lakini kuna wageni wanaoingia na kutoka ambao hao ni wengi sana kwa kuwa wakuja kununua madini na watu hawa hawana makazi ya kudumu, wapo wanaonunua nyumba za wenyeji ambazo zinakwisha sasa, hivyo NHC mkiweza kujenga hapa itasaidia kupunguza adha ya nyumba katika Wilaya na Mkao kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Zahra Michuzi amesema kuwa wako tayari kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo lakini pia amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuendelea kutoa huduma bora katika sekta ya ujenzi na hivyo kuwafanya watanzania wajivunie na Shirika lao.
 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here