Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ameshiriki kwa njia ya mtandao Mkutano wa Mapinduzi ya kijani Barani Afrika (Africa Green Revolution Forum) akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mkutano uliofanyika Jijini Nairobi Nchini Kenya umehudhuriwa na Viongozi wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi wa Mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Katika Mkutano huo Mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwemo uwekezaji wa kifedha katika kutekeleza mapinduzi ya sekta ya kilimo barani afrika, kuwezesha ugunduzi(uvumbuzi) katika sekta ya kilimo barani afrika, ushiriki wa wanawake katika kilimo pamoja ugunduzi na uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali zinazogusa sekta ya kilimo barani Afrika.
Mkutano huo pia umejadili Masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya Uviko 19 katika upatikanaji wa Chakula kwa Nchi za Afrika pamoja na Athari za mabadiliko ya Tabia ya Nchi katika kilimo na biashara ya Kilimo barani Afrika
Akijibu swali kutoka kwa muongozaji wa Mkutano huo juu ya yale yatakayowasilishwa na Tanzania katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mfumo wa Upatikanaji Chakula “ UN Food System Summit “ unaotarajiwa kufanyika Septemba 23, 2021 Makamu wa Rais amesema Tanzania itawasilisha masuala ya uwezeshaji wa kifedha katika sekta ya kilimo, suala la ukosefu wa mbegu bora za mazao ya Kilimo na Uvuvi, Changamoto za wadudu haribifu wa mazao pamoja na ukosefu wa teknolojia za kisasa katika masuala ya kilimo na ufugaji.
Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuinua kilimo nchini ikiwemo sera ya kilimo ya mwaka 2013 pamoja na kuboresha mpango wa maendeleo ya kilimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa mwaka 2020-2029.