Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao akitoa maelezo mafupi kuhusu Mkutano wa mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Jijini Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo.
Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mhe. Neema Lugangira,akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulioanza leo September 29,2021 Jijini Dodoma.
Mrajis wa Jumuiya ya zisizo za kiserikali Zanzibar Ahmed Abdulla,akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulioanza leo September 29,2021 Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee nwakati wa Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulioanza leo September 29,2021 Jijini Dodoma. |
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akitoa tuzo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT Brenda Msangi kwa mchango wa Shirika hilo kutoa ajira nyingi katika Jamii.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua semina ya Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ulioanza leo September 29,2021 Jijini Dodoma.
DODOMA.
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dkt.Doroth Gwajima,amesema kuwa nia ya Serikali ni kuendelea kujenga pamoja na kuboresha mazingira wezeshi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.
Hayo ameyasema leo September 29,2021 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Gwajima amesema Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na NGOs katika kuisaidia Serikali ili kuwaletea wananchi Maendeleo.
“Mashirika yanakwenda hatua kwa hatua na Serikali na hata Maendeleo haya tuliyonayo na hapa tulipofika ni kutokana na mchango mkubwa wa Mashirika haya” amesema Waziri Gwajima.
Dk. Gwajima amefafanua kuwa fursa muhimu ya kujadiliana masuala mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo kuyajengea uwezo Mashirika hayo kuhusu sheria na kanuni zinazoongoza NGOs na Serikali pia kufahamu changamoto na shughuli zinazofanywa na NGOs ili kuwa na uelewa wa Pamoja.
Aidha, Mhe. Gwajima ametoa wito kwa NGOs kuimarika kwa kufanya kazi kwa weledi na uzalendo, kufuata sheria na kanuni zake kwa manufaa ya Taifa na kwamba Serikali ipo tayari kupokea maoni na changamoto kupitia Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaani NaCONGO.
Hata hivyo ameeleza kuwa, NGOs zifanye kazi kwa uwazi na uwajibikaji kwenye mipango yao ya kila mwaka hususani kuanzia kwenye maeneo wanayofanyia kazi.
Aidha Dk. Gwajima ameyataka Mashirika hayo kushirikiana na Serikali kufikisha elimu ya chanjo ya ugonjwa wa Uvico 19 kwa wananchi huku akisisitiza chanjo hiyo ni ya hiari kama alivyosisitiza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Waziri Gwajima amesema suala la chanjo ni hiari na Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza katika mikutano yake hivyo Mashirika hayo yanawajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na jambo hilo.
“Napenda kusisitiza pia na kuwakumbusha kwamba chanjo hii ni hiari na Mheshimiwa Rais amekuwa akikumbusha kila mara anapoenda kwenye mikutano yake na kuwakumbusha watanzania wajitokeze wakachanje kwa hiari.
“Nia yake Rais ni kuona Taifa lipo salama na Uvico 19 kwa kutekeleza afua za kinga ikiwemo afua ya chanjo kwa hiari” amelisisitiza.
Hivyo nitumie nafasi hii kuwakummbusha nyinyi kama wadau wenye majukumu mbalimbali na uelewa wenu mkubwa na uzoefu wenu mkashirikiane na wataalamu wetu wa afya na sekta zote mkasimamie na kuwezesha suala la elimu.
“Elimu itolewe kwa wananchi na suala la dhana ya uhiari likafanyike vizuri kwa kuwekeza kwenye msingi wa elimu kama alivyosema mheshimiwa Rais.
“Ikatokea mahala watu wengine wakataka kupotosha nia njema ambayo Rais amesema bahati nzuri wale watu wakaomba msamaha tulishasema speech za viongozi ni suala nyeti kabla hujaamua kutoka nayo hakikisha umeilewa,”amesema.
Aidha,Waziri Gwajima amewashukuru wananchi kwa jinsi ambavyo wameipokea kampeni hiyo ambapo amedai Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huo.
“Wizara itaendelea kushirikiana nanyi katika kutekeleza dhamira kubwa ya Rais ya elimu kukubaliana na UVICO 19.Mashirika yasiyokuwa yakiserikali mshirikiane na kule chini ili kila sikio likasikie ili kutekeleza afua hii,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO) Dkt. Lilian Badi amempongeza Waziri Gwajima Kwa kufanikisha uchaguzi wa NaCONGO na kusema kuwa ni wakati wa kufungua macho na kuboresha utendaji kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kuongeza Kasi ya Maendeleo.
Awali Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema lengo la Mkutano huo ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa NGOs na Serikali kwa kujadiliana changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua kwa kuzingatia Sheria na Sera zilizopo.
Aidha, Mkutano umelenga kutambua na kujadili mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mhe. Neema Lugangira ameiomba Serikali kufanya mapitio ya kanuni ya fedha ya NGOs kuwezesha kupata vibali mapema ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Credit – Fullshangwe Blog.