Na: Maiko Luoga Kilimanjaro.
Askofu mkuu wa kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Dkt, Maimbo Mndolwa ameongoza waumini wa kanisa hilo na washiriki wa safari ya msalaba inayoendelea katika Dayosisi hiyo kuwaombea wanafunzi wanaotarajia kuanza mitihani siku chache zijazo ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na vyuo mbalimbali nchini.
Ibada ya maombi hayo imefanyika septemba 05/2021 huko katika kijiji cha Mamba myamba wilayani Same mkoani Kilimanjaro mara baada ya washiriki hao wa safari ya msalaba, kufanya mkesha wa siku moja kijijini hapo kisha kuendelea na safari wakitembea kwa miguu kutoka Buiko kuelekea Magila Msalabani mkoani Tanga.
“Tunafanya maombi haya ili kuwaombea kwa Mungu watoto wetu wanaotarajia kuanza mitihani yao ili wafanye vizuri kila mmoja kwa darasa lake wakiwemo wale wa Darasa la saba, kidato cha nne, vyuo na wote wanaojiandaa kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu Mungu awatangulie” Dkt, Mndolwa Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania.
Pamoja na maombi hayo Askofu Mndolwa amewataka wazazi na walezi kote nchini kutimiza vema majukumu ya kulea familia zao ili kusaidia watoto kukua katika misingi bora ya kumpendeza Mungu badala ya kuwaacha na wafanyakazi wa ndani kila wakati ambao mara nyingi wasio waaminifu huwafanyia vitendo vya kikatili watoto hao bila wazazi kujua.
“Unakuta mzazi kila siku anamuacha mwanae mdogo na mfanyakazi wa ndani bila kufuatilia mazingira yake ya maisha, madhara ya jambo hili ni makubwa maana huyo mfanyakazi kama sio mwaminifu anaweza kumfanyia mwanao jambo lolote liwe jema au baya maana wewe huna muda na mwanao” alieleza Askofu Mndolwa.
Kwa upande wao Makasisi walioshiriki maombi hayo akiwemo Canon Christopher Kiango na Canon Charles Lundu wamesema, yatawasaidia watahiniwa kujiamini wawapo kwenye vyumba vya mitihani wakitanguliza mbele hofu ya Mungu na kufanya vizuri kwenye mitihani yao.