Home BUSINESS ZAIDI YA TANI 70 ZA DAWA FEKI ZA SULPHER ZAKAMATWA TUNDURU.

ZAIDI YA TANI 70 ZA DAWA FEKI ZA SULPHER ZAKAMATWA TUNDURU.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kulia, akimuonesha Naibu Waziri wa Kilimo Hussen Bashe sehemu ya Dawa  feki ya kupulizia korosho(Sulphur) iliyokamatwa ikiuzwa kwa wakulima wa korosho katika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambayo Kama ingesambazwa ingeleta athari kubwa kiuchumi kwa wakulima wa zao hilo.(Picha na Muhidin Amri).
 
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kulia, akimuonesha Naibu Waziri wa Kilimo Hussen Bashe sehemu ya Dawa feki ya kupulizia korosho(Sulphur) iliyokamatwa ikiuzwa kwa wakulima wa korosho katika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambayo Kama ingesambazwa ingeleta athari kubwa kiuchumi kwa wakulima wa zao hilo. (Picha na Muhidin Amri).

Na: Muhidin Amri,Tunduru
SERIKALI wilayani Tunduru imekamata zaidi ya tani 70.2 sawa na mifuko 70,200 ya dawa feki ya Sulphur ya kupulizia mikoroshoiliyokuwa inauzwa kwa wakulima katika wilaya hiyo.

Aidha, wafanyabiashara wawili  wanashikiliwa na vyombo vya dola kuhusiana na uingizaji wa dawa hizo feki ambazo  kama zingewafikia wakulima wengi, zingeshusha uzalishaji wa korosho kwa msimu wa mwaka 2021/2022 na kusababisha umaskini  kwa wakulima na halmashauri kukosa mapato.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, alibainisha hayo  hivi karibuni alipokuwa akitoa taarifa ya maandalizi ya msimu mpya wa korosho kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Alisema kukamatwa kwa dawa hizo feki kumetokana na msako unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo dhidi ya watu wanaoingiza dawa feki na kwa njia za magendo ambao wamekuwa chanzo cha kushuka kwa uzalishaji wa korosho na mazao mengine katika mashamba.

Kwa mujibu wa Mtatiro, dawa hizo za unga zilichanganywa na pumba za mpunga na kufungwa kwenye mifuko ya kampuni moja inayoingiza pembejeo za kilimo hususani sulphur hapa nchini.

Alisema hilo ni tatizo kubwa na kuiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya watu hao wanaohatarisha uchumi wa wilaya ya Tunduru na nchi kwa jumla.

Kwa upande wake,Naibu Waziri Bashe aliagiza wafanyabiashara waliohusika na kuuza sulphur hiyo wafunguliwe kesi ya uhujumu uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia wakulima wote waliouziwa dawa hiyo.

Bashe alisema kitendo cha wakulima kuuziwa sulphur hiyo ni uhujumu uchumi na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kuorodhesha wakulima wote walionunua dawa hiyo ili wadai fidia kutokana na hasara waliyopata.

Alisema uzalishaji wa korosho umekuwa unashuka mwaka hadi mwaka kutokana na wakulima kuuziwa pembejeo feki ambazo zimekuwa chanzo cha kushuka kwa zao hilo katika mikoa mbalimbali nchini.

Aidha, Bashe aliitaka Taasisi ya Viuatilifu Tanzania (TPRA) kufungua ofisi zao hadi ngazi ya wilaya ili kuwa na uwezo wa kufanya ukaguzi wa pembejeo mara kwa mara na wale watakaokutwa wanauza pembejeo feki,licha ya kufikishwa mahakamani na wafutiwe leseni zao.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,  Brigadia Jenerali Wilbet Ibuge alisema tatizo la viuatilifu feki vinavyouzwa kwa wakulima ni sababu mojawapo inayowasumbua wakulima.

Jenerali Ibuge alisema, Serikali ya Mkoa wa Ruvuma itahakikisha inakata mnyoyoro wa wauzaji feki wa pembejeo.

Aliwataka wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo kufanya operesheni ya kuwakamata wafanyabiashara wanaoingiza na kuuza pembejeo feki kwa wakulima.

Previous articleMHE. SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO TLS NA TAWJA.
Next articleUMOJA WA AFRIKA KUIPATIA TANZANIA CHANJO MILIONI 17 ZA UVIKO 19

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here