Home LOCAL WAZIRI WA TAMISEMI AKAGUA BARABARA NJENGERENDETI HADI UTALINGOLO NJOMBE MJINI.

WAZIRI WA TAMISEMI AKAGUA BARABARA NJENGERENDETI HADI UTALINGOLO NJOMBE MJINI.

 Na: Maiko Luoga, NJOMBE 

Wananchi wa kata ya Utalingolo Halmashauri ya Mji na mkoa wa Njombe  kupitia Diwani wa kata hiyo Mhe, Erasto Mpete wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea watumishi kumi wa Afya katika kituo cha Afya kata ya Utalingolo kilichopo katika kijiji cha Ihalula.

Walitoa shukrani hizo Agosti 10/2021 mbele ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe, Ummy Mwalimu aliyefika katani hapo akiwa kwenye ziara ya kikazi kukagua miundombinu ya barabara ya kutoka eneo la Njengerendete hadi Utalingolo inayosimamiwa na wakala wa barabara za mijini na Vijijini TARURA Halmashauri ya Mji wa Njombe.

“Tunaishukuru sana Serikali chini ya Mhe, Rais mama Samia Suluhu Hasan, Mhe, Waziri na Mbunge wetu Deo Mwanyika  kutuletea watumishi kumi katika ajira mpya na kuwapeleka moja kwa moja kwenye kituo chetu cha Afya kata ya Utalingolo kilichopo kwenye kijiji cha Ihalula, pia niliwashukuru TARURA kwa kutusaidia barabara kwa kiwango cha changarawe kwa sehemu zilizokuwa korofi hasa eneo la Mfereke” alieleza Erasto Mpete.

Pamoja na shukrani hizo Diwani wa kata ya Utalingolo na makamu mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Mhe, Erasto Mpete alitumia nafasi hiyo kuwasilisha kilio cha wananchi kwa Waziri wa TAMISEMI juu ya ukosefu wa gari la wagonjwa na ukosefu wa watalaamu wa vipimo vya Utrasound na X-ray katika Kituo hicho cha Afya katani hapo.

Aidha Mpete alisema barabara ya Utalingolo ni kiunganishi cha kata tano zinazoitegemea kwa uchumi hivyo ni vyema iimarishwe zaidi ili kuhudumia jamii kubwa ya wananchi huku akiomba barabara ya kwenda kituo cha Afya kata ya Utalingolo kilichopo Ihalula kupitia Mfereke ijengwe kwa kiwango cha lami.

“Pamoja na haya Mhe, Waziri tunaomba sana tusaidiwe huduma ya umeme hasa Kijiji cha Mfereke ambacho kipo karibu na chuo cha Katoliki kilichopo hapo Kijijini, zinahitajika wastani nguzo saba tu ili umeme ufike Zahanati, kijiji cha Utalingolo, meneja wa TANESCO alisema watapata awamu hii” aliongeza Mhe, Erasto Mpete.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumsikiliza na kujibu hoja zao zilizowasilishwa kwake na Diwani wa Kata ya Utalingolo Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe, Ummy Mwalimu alisema hawezi kuahidi gari la wagonjwa kwa sasa kituoni hapo kwa kuwa ameshaahidi kutoa gari katika Kituo cha Afya kata ya Makowo hivyo Serikali imeipokea changamoto hiyo na kuahidi kuitatua hapo baadae.

Kuhusu ukosefu wa wataalamu wa mashine za X-ray na Ultrasound mhe, Ummy Mwalimu alisema amelichulua jambo hilo ili kulifanyia kazi huku akiagiza TARURA kuhakikisha barabara ya Njengerendete inaboreshwa ili kukidhi mahitaji ya wananchi.  

“Kwasasa serikali itaanza ujenzi wa barabara ya lami kipande cha kilomita nne za kuanzia na eneo linalobaki TARURA wataliweka katika ubora hadi Kituo cha Afya cha kata ya Utalingolo kuhusu umeme Mfereke jambo hili nitalifikisha kwa waziri husika ili liweze kupatiwa ufumbuzi” alieleza Mhe, Ummy Mwalimu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Ujio wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe, Ummy Mwalimu katika Jimbo la Njombe mjini ni matokeo chanya ya ziara ya Mbunge wa jimbo hilo Mhe, Deo mwanyika aliyoifanya kuanzia julai 2021 akipita katika kata za jimbo hilo kwa lengo la kuzungumza na wananchi na kupokea kero zao hatimae kuzifikisha Serikalini ili zipatiwe ufumbuzi.

Previous articleTANZANIA YAPATA MISS, MR. VIZIWI.
Next articleRAIS SAMIA SULUHU HASSAN AONDOKA NCHINI KUELEKEA MALAWI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here