Home BUSINESS WAKULIMA WA MBAAZI WAENDELEA KUVUNA FEDHA,WANUNUZI PIGANA VIKUMBO NA KUPANDISHA BEI

WAKULIMA WA MBAAZI WAENDELEA KUVUNA FEDHA,WANUNUZI PIGANA VIKUMBO NA KUPANDISHA BEI

Baadhi ya wakulima wakifuatilia mnada wa mbaazi  zinazouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma jana.

Baadhi ya vijana  kutoka maeneo mbalimbali wa wilaya ya Namtumbo waliopata vibarua vya muda wakishusha shehena ya mbaazi  wakati wa mnada wa tatu wa zao  hilo uliofanyika Namtumbo. (Picha na Muhidin Amri).

Na: Muhidin Amri,Tunduru.

CHAMA Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma (Tamcu td),kimefanya mnada wa pili wa zao  la mbaazi  kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo katika mnada huo jumla ya kilo 1,145,498 zimeuzwa.

Mnada huo umefanyika katika kijiji cha Semeni kupitia Chama cha Msingi Asema Amcos  ambapo makampuni matano yamejitokeza kununua mbaazi na kampuni ya Lenic Tanzania Ltd imeshinda  kununua kwa bei ya Sh.1,344 kwa kilo.

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU LTD)Imani Kalembo amesema, huo ni mnada wa pili  wa zao la mbaazi kufanyika katika wilaya hiyo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021.

Amesema, katika mnada huo jumla ya tani 1,042 sawa na kilo 1,145,498 zimeuzwa ambapo bei ya kilo moja  ya mbaazi ni Sh  1,344.

Kalembo amesema,ni furaha kama Chama Kikuu cha Ushirika kuona bei ya mbaazi  inaongezeka kila mnada kwani katika mnada wa kwanza uliofanyika  katika kijiji cha Mtonya bei  ilikuwa Sh 1,294,lakini katika mnada  wa pili bei imefikia Sh 1,344.

Amewataka wakulima kutokubali kushawishika na wanunuzi wa kati wanaonunua mbaazi kwa bei ndogo ya Sh 800 kwa kilo ambayo haina faida, badala yake kuendelea kuuza mbaazi zao  mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia vyama vya msingi vya ushirika.

Ametoa rai kwa makampuni  mbalimbali,kwenda katika wilaya hiyo kununua mbaazi ambazo zinapatikana kwa wingi na kuhakikisha wananunua kwa bei nzuri ili kuhamasisha wakulima waweze kuzalisha kwa wingi.

Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru Georg Bisani amesema,katika minada yote miwili jumla ya kilo 1,505,849 zimeuzwa ambapo katika mnada wa kwanza zimeuzwa kilo 360,531 kwa bei ya chini ya Sh. 1,277 huku bei ya juu ilikuwa Sh.1,294.

Amesema, katika mnada wa pili uliofanyika jana katika kijiji cha Semeni jumla ya kilo 1,145,498 zimeuzwa kwa bei ya Sh.1,344 na kufanya jumla ya fedha zote zilizoingia kwenye mzunguko kutokana na minada  yote miwili ya mbaazi wilayani Tunduru kuwa Sh. Bilioni 1,536,167,320.00.

Wakulima wa mbaazi katika kijiji hicho wameishukuru  Serikali kwa kuliingiza zao  hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa umewasaidia  kupata soko la uhakika na bei nzuri ikilinganishwa na  siku za nyuma ambapo wafanyabiashara walinunua kwa bei ndogo  kati ya Sh 250  na 300.

Wamesema, kuanzishwa kwa  mfumo wa stakabadhi ghalani kwa zao la mbaazi na mazao mengine ya kimkakati ikiwemo zao maarufu la korosho kumewasaidia  kuwa na uhakika wa bei nzuri na kuepuka kulanguliwa na wanunuzi wa mitaani wasiokuwa  na huruma kwao.

Hadija Omari(43)amesema, kama serikali itaendelea na kusimamia mpango wa kuuza mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani basi wakulima wengi watahamasika kuongeza uzalishaji na hivyo kuondokana na umaskini katika familia zao.

Hata hivyo, ameiomba Serikali kuhakikisha inawabana na kuwachukulia hatua kali baadhi ya wanunuzi wachache wanaopita mashambani na vijijini kuwalaghai wakulima ili wauze mbaazi kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi za uzalishaji.

Mkulima mwingine Omari Misoya amesema, licha ya malipo kuchelewa  mara wanapouza,lakini mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kupata bei nzuri ya mbaazi wanazolima ikilinganisha na bei za walanguzi wa mitaani.

Amesema,mfumo  huo umeleta heshima kubwa  kwa mkulima na pia usalama wa fedha wanazolipwa kwani zinapitia moja kwa moja benki badala ya kupewa mkononi jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

Ameitaka Serikali kupitia wizara ya kilimo kuyabana makampuni yanayonunua  mbaazi kulipa fedha  kwa wakulima haraka ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili kwenye familia zao  ikiwemo mahitaji ya shule kwa Watoto wao.
MWISHO.

Previous articleDC ILALA AZITAKA BODI ZA SHULE ISIWE UWANJA WA SIASA
Next articleMAGAZETI YA LEO J.TANO SEPTEMBA 1-2021.
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here