Home ENTERTAINMENTS TANZANIA YAPATA MISS, MR. VIZIWI.

TANZANIA YAPATA MISS, MR. VIZIWI.

NA: HERI SHAABAN, Dar es Salaam.

Hadija Kanyauma na Rajan Ally wameibuka washindi katika mashindano ya kumtafuta mrembo wa Tanzania kwa watu wenye uziwi hivyo wataiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Mashindano hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania.

Akizungumza wakati wa mashindano hayo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Dk. Emmanuel Ishengoma ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema ni fursa nzuri kwa watu wenye uziwi kuonyesha vipaji vyao.

“Kila mmoja ana kipawa cha ziada, mtu anaweza kuwa na ulemavu wa macho au kushindwa kusikia lakini akawa na kipaji. Washiriki wote ni wazuri na Tanzania inaweza kutoa mshindi wa Afrika,” amesema Dk. Ishengoma. 


Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania, Habibu Mrope, amesema kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikaribishwa katika mataifa mengi kushiriki mashindano hayo lakini walikuwa wakishindwa kutokana na changamoto mbalimbali.

“Tuliangalia namna ya kusukuma jambo hili lisiendelee kulala ndiyo maana tukawa na mashindano haya. Wapo viziwi warembo na wanafanya vizuri kwahiyo tunaamini hata katika mashindaano ya kimataifa Tanzania tutafanya vizuri,” amesema Mrope.

Aidha amesema washindi watakabidhiwa zawadi zao mwezi ujao ambapo mshindi wa kwanza atakabidhiwa samani na fedha taslimu Sh milioni moja wakati mshindi wa pili atakabidhiwa Sh milioni moja.

Katika mashindano hayo pia kituo hicho kilitoa tuzo kwa watu mbalimbali kwa kutambua mchango wao katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viziwi katika shughuli zao za kila siku.

Mbali ya Hadija na Rajan pia kulikuwa na washindi katika kipengele cha mwanamitindo bora.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here