Home LOCAL TAKUKURU YAPEWA RUNGU KUSHUGHULIKIA WALIOGEUZA TARIME SHAMBA LA BIBI

TAKUKURU YAPEWA RUNGU KUSHUGHULIKIA WALIOGEUZA TARIME SHAMBA LA BIBI

Na: Mwandishi wetu, TARIME.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara imetakiwa kuchunguza miradi ya maendeleo iliyotiliwa shaka na Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Tarime Leo.

RC Hapi amesema maishani mwake hakuwahi kushuhudia uozo kama aliyokutana nao kwenye miradi aliyokagua ikiwamo ya ujenzi wa Shule ya Msingi Ntimaro, Shule ya Sekondari Nyamongo na Kituo cha Afya cha Nyamongo.

Amemtaka Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa huo, Hassan Mossi kuweka kambi wilayani humo kuhakikisha habakizi hata Mtu mmoja aliyekula fedha za miradi hiyo na kwamba akihisi wanaweza kukimbia awakamate na kuwaweka ndani.

“Ikiwa unahitaji kuimarishiwa timu yako niambie niwasiliane na Kamishna haraka, nataka kazi hii ifanywe kwa kasi kubwa ili tunusuru fedha za wananchi na kazi ziendelee,” amesema RC.

Katika Kijiji cha Kerembe ilikojengwa Shule ya Msingi ilielezwa na Mtendaji wa Kijiji hicho, Mogosi Ntambe kuwa walipokea jumla ya Sh milioni 870 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

RC Hapi baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa madarasa Saba, ofisi na nyumba Nne za walimu, ameagiza uchunguzi ufanywe katika miradi yote  kutekelezwa kwa kutumia fedha hiyo.

Kwa upande wa Sekondari ya Nyamongo, ujenzi wa madarasa matatu haujakamilika huku zikiwa zimetumiwa Sh milioni 80. 

Aidha ilibainika ununuzi wa vifaa ulifanywa holela katika halo ya kunufaisha wauzaji kwani Nondo 900 na Mifuko 1000 ya simenti imebaki na imeanza kuganda.

“Halmashauri hii ilikuwa imeoza tutaomba mamlaka zinazohusika zitusaidie kuifumua ili kila aliyehusika na mtandao wa ulaji fedha za miradi atupishe,” amesema RC

Amesema kwingine mradi unaohusisha ujenzi wa jengo la madarasa mawili na ofisi ya walimu likiwa limewekwa umeme, sakafu ya vigae, dari ya gypsum na madarasani kukiwa kumewekwa viti na meza 20 unagharimu Sh milioni 40 lakini Tarime madarasa matatu hayajakamilishwa na Sh milioni 80 zimekwisha.

Kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamongo kumekutwa yamebakia matofali sawa na  yaliyojenga kituo hicho hali iliyotafsiriwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here