Dodoma: Tarehe 31 Agosti, 2021:
Tarehe 19 Julai, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliwaelekeza Waheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kupitia upya tozo za miamala ya simu baada ya kusikia kilio cha wananchi kuhusu tozo hizo.
Katika kutekeleza Maelekezo hayo, leo tarehe 31 Agosti, 2021, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametia saini marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Kieletroniki za Kutuma na Kutoa Fedha za Mwaka 2021 na kupunguza viwango vya tozo za miamala hiyo kwa asilimia 30. Aidha, Serikali imefanya majadiliano na watoa huduma za simu ambao nao wameridhia kupunguza viwango vya tozo wanazotoza katika miamala ya kutuma na kutoa fedha kati ya mtandao na mtandao mwingine kwa asilimia 10.
Viwango vilivyopunguzwa vitatangazwa rasmi kwa Tangazo la Serikali kesho tarehe 1 Septemba, 2021.
Serikali inaamini kuwa uamuzi huo utatoa nafuu kwa wananchi na kuiwezesha Serikali kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyokusudiwa wakati tozo hizo ziliporidhiwa na kupitishwa na Bunge la Bajeti la Mwaka 2021/2022.
Ni imani ya Serikali kwamba wananchi wataunga mkono uamuzi huu kwani tozo hizo zimeanza kuleta manufaa makubwa kwa wananchi ikiwemo kiasi cha shilingi bilioni 48.4 zilizokusanywa hivi karibuni ambazo zimeelekezwa katika kujenga vituo vya afya 150 na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 560 nchi nzima.