Home BUSINESS SERIKALI KUSITISHA VIBALI VYA UAGIZAJI WA SUKARI IFIKAPO 2022-WAZIRI MKENDA

SERIKALI KUSITISHA VIBALI VYA UAGIZAJI WA SUKARI IFIKAPO 2022-WAZIRI MKENDA

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kongamano la saba la wadau wa sekta ya kilimo kuhusu sera pamoja na kutathmini shughuli za kilimo nchini, leo tarehe 5 Agosti 2021 linalofanyika katika ukumbi wa Asante Estates uliopo katika eneo la Ntyuka Jijini Dodoma.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la kuendeleza kilimo kusini mwa Tanzania SAGCOT akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kongamano la saba la wadau wa sekta ya kilimo kuhusu sera pamoja na kutathmini shughuli za kilimo nchini, leo tarehe 5 Agosti 2021 linalofanyika katika ukumbi wa Asante Estates uliopo katika eneo la Ntyuka Jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa kongamano la saba la wadau wa sekta ya kilimo kuhusu sera pamoja na kutathmini shughuli za kilimo nchini, linalofanyika katika ukumbi wa Asante Estates uliopo katika eneo la Ntyuka Jijini Dodoma wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati wa kongamano hilo.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali imesema ifikapo Mwaka 2022 itasitisha utoaji wa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kwa makampuni ambayo ndio wazalishaji wa ndani wa bidhaa hiyo.

Upungufu wa bidhaa hiyo nchini hautokani na uhaba wa miwa bali unasababishwa na makampuni kushindwa kuongeza uchakataji wa miwa kutoka kwa wakulima.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 5 Agosti 2021 katika ukumbi wa Asante Estates uliopo katika eneo la Ntyuka Jijini Dodoma aliposhiriki katika kongamano la saba la wadau wa sekta ya kilimo kuhusu sera pamoja na kutathmini shughuli za kilimo nchini.

“Baada ya mwaka huu Serikali haitotoa vibali kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya sukari kuagiza sukari nje kwani tayari watakuwa wamefikia uwezo wa kuzalisha sukari toshelevu ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa uanzishwaji wa viwanda vipya vya sukari hapa nchini”

Waziri Mkenda amesema kuwa zaidi ya Tani 350,000 za miwa ya wakulima katika Bonde la Kilombero mkoani Morogoro zinateketezwa kwa moto kutokana na kukosa soko la uhakika lakini viwanda haviongezi uwezo wa kuchakata miwa ili kuzalisha sukari ya kutosha.

Amesema kuwa zaidi ya Tani 40,000 zinaagizwa kutoka nje ya nchi jambo ambalo sio sahihi kwani viwanda vya sukari vilivyopo nchini vinapaswa kuongeza uwezo wao ili kuimarisha soko la wakulima jambo litakalopelekea nchi kutoagiza sukari.

Waziri Mkenda amesema kuwa mtu yeyote atakayeingiza sukari kiholela ni wasaliti wa nchi hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema kuwa kuna wimbi kubwa la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana lakini viwanda vimeshindwa kuongeza uwezo wake wa kuzalisha sukari ili kuimarisha sekta ya ajira kwa wananchi.

Katika mkutano huo Waziri Mkenda ameipongeza serikali na mawaziri waliotangulia kuiongoza Wizara ya Kilimo kwa kusimamia vyema sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kufanikisha kupunguza wimbi kubwa la uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here