Home LOCAL RUKWA KUPOKEA CHANJO DOZI 20,000 ZA UVIKO-19: DKT. KASULULU

RUKWA KUPOKEA CHANJO DOZI 20,000 ZA UVIKO-19: DKT. KASULULU

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dk. Boniface Kasululu (kushoto) akiongea na viongozi wa hospitali ya Dk.Atiman leo alipokwenda kukagua maandalizi ya zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 kwa wananchi wa Sumbawanga litakaloanza Jumatano wiki hii.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu (katikati) akiwa na wataalam wa Mkoa leo alipokagua maandalizi ya zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 kwenye kituo cha Afya Mazwi Manispaa ya Sumbawanga.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga kukagua wa eneo litakalotumika kutoa chanjo ya UVIKO kwa wananchi waliojisajili wa Wilaya ya Sumbawanga. 
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

 RUKWA.

Mkoa wa Rukwa umekamilisha maandalizi ya mapokezi ya chanjo za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ambapo jumla ya vituo 11 vitatumika kote mkoani kuchanja watu watakaokuwa wamejiandikisha kwa hiari kuanzia Jumatano wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo (02.08.2021) Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akiwa kwenye ziara ya kukagua vituo vya kutolea chanjo hiyo kwenye Manispaa ya Sumbawanga alibainisha utayari wa mkoa kutekeleza zoezi hilo muhimu katika kukabiliana na janga la UVIKO-19

“Maandalizi ya mapokezi ya dozi 20,000 za UVIKO 19 zilizotengwa kwa ajili ya watu wa mKoa wa Rukwa yamekamilika na kuwa sasa tunasubiri uzinduzi rasmi wa kuchanja wote waliojisajili kwa hiari yao ambapo Mkuu wa Mkoa wetu Joseph Joseph Mkirikiti atazindua zoezi hilo siku ya Jumatano wiki hii” alisema Dkt. Kasululu.

Aliongeza kusema ili mwananchi aweze kupatiwa chanjo hiyo atapaswa kujisali kwenye mfumo uliowekwa na Wizara ya Afya kupitia tovuti yake na au aende kwa moja kwenye kituo kitakachotumika kwenye zoezi hilo

Dkt. Kasululu ametaja vituo vitakavyotumika kwa zoezi la chanjo ya UVIKO 19 kwa awamu ya kwanza kwenye Manispaa ya Sumbawanga kuwa ni Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga, Hospitali ya Dr.Atiman na Kituio cha Afya Mazwi.

Kwa upande wa Wilaya ya Nkasi chanjo itatolewa kwenye vituo vitatu ambayo ni hospitali ya Misheni Namanyele, Kituo cha Afya Nkomolo na Kituo cha Afya Kilando.

Wilaya ya Kalambo chanjo ya UVIKO 19 itatolewa kwenye vituo viwili ambavyo ni Kituo cha Afya Matai na Kituo cha Afya  Mwimbi.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Kasululu alitaja vituo vitatu ambayo vitatoa chanji hiyo ya UVIKO kuwa ni Kituo cha  Afya Laela, Kituo cha Afya Mpui na Kituo cha Afya Mtowisha.

Aidha, chanjo itatolewa pia kwa wananchi wa Wilaya za Nkasi, Kalambo na Laela ambapo Dkt. Kasululu amebainisha kuwa tayari watoa huduma za afya kwenye maeneo wamejengewa uwezo kutekeleza jukumu hilo.

Kuhusu taarifa potofu kuwa chanjo ina madhara, Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa alisema wananchi wasiwe na hofu kwani chanjo inayotolewa imethibitishwa pasipo shaka juu ya ubora wake na kuwa serikali ipo makini kuwalinda watu wake.

“Nami zoezi litakapozinduliwa hapa mkoani nitakuwa wa kwanza kuchanja kwa kundi la watumishi wa afya ,hivyo nawathibitishia kuwa chanjo hii ya UVIKO 19 ni salama” alisisitiza Dkt. Kasululu.

Makundi ambayo yanalengwa kufikiwa na dozi 20,000 za awamu ya kwanza mkoa wa Rukwa ni watumishi wa afya, watu wenye umri zaidi ya miaka 50 na tatu watu wenye matatizo ya mfumo wa damu (BP),Pumu,Kisukari na matatizo ya moyo  ambao wamethibitishwa na wataalam .

Mwisho

Imeandaliwa na;

Afisa Habari Mkuu,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,

SUMBAWANGA

02..08.2021

Previous articleMHE. RAIS SAMIA ASHIRIKI CHAKULA CHA JIONI NCHINI RWANDA
Next articleTMDA YATOA ELIMU KWA WANANCHI JUU YA CHANJO ZA UVIKO-19

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here