Home LOCAL KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI INAYOSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU...

KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI INAYOSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA ZANZIBAR YAFANYA ZIARA KISARAWE-PWANI

 
Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar, wakiangalia shimo la mabaki ya majivu yaliotokana na taka hatarishi zilizochomwa kiwandani hapo.

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar, wakipata maelezo kutoka kwa Bi.Maimuna Salum Mkurugenzi wa Mazingira na Taka Hatarishi Tindwa Medical and Health Service Kisarawe Mkoa wa Pwani.

Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe. Saada Mkuya (katikati), akizungumza baada ya kufanya ukaguzi pamoja na kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi katika kiwanda cha Tindwa Medical and Health Service kilichopo Kisarawe Pwani.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar, wakisikiliza maelezo yanayotolewa na Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Saada Mkuya (hayupo pichani).

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar yafanya ziara Kisarawe Mkoa wa Pwani kwenye mitambo ya kuchomea taka hatarishi katika Kiwanda cha Tindwa Medical and Health service, ili kujionea namna wanavyochoma taka hizo bila ya kuathiri Mazingira.

Kamati hiyo imeambatana na Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe. Saada Mkuya, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dkt. Omary Shajaak, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Mtumwa Peya pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Mhe.Saada Mkuya amesema kuwa lengo la kufanya ziara ni kujifunza jinsi gani wanaweza kutunza na kuteketeza taka hatarishi kutoka Hospitalini na Viwandani bila ya kuathiri mazingira. Ameeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar kuna changamoto kubwa katika kuteketeza taka hatarishi hivyo wametumia fursa hii kuja kujifunza namna gani watachoma na kuteketeza taka hizo.

“kwa upande wa Zanzibar tuna changamoto kubwa katika kuhifadhi na kuteketeza taka hatarishi kwa mfano tuna Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ambayo ndio pekee inateketeza taka hizo na muda mwengine kupelekea kuelemewa na kushindwa kufanya kazi zake kwa ufasihi”. Amesema Mhe. Saada

Ameendelea kusema kuwa Zanzibar ni kisiwa cha utalii na inafahamika kuwa utalii unaendana na hali ya mazingira na usafi na kama tutashindwa kuhifadhi na kutunza mazingira yetu kwa kiasi kikubwa tutapunguza ubora wa utalii. Hivyo tumekuja hapa kujifunza na itatusaidia kuweka miongozo ya namna gani ya kuhifadhi na kuteketeza taka hizo bila ya kuharibu mazingira.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar Mhe. Mtumwa Peya amesema kuwa, ziara hii ya kamati katika kiwanda cha Tindwa imewapa fursa ya kujifunza kwani kwa upande wa Zanzibar bado kiwanda kikubwa cha kuunguza taka hatarishi bado hakipo.

“Kwa upande wetu Zanzibar hatuna kiwanda kama hiki hivyo kupelekea taka kuzagaa hovyo na kuharibu mazingira, mimi nikiwa kama kaimu Mwenyekiti wa Kamati hii nimefarijika sana kuona kiwanda hiki namna wanavyoteketeza taka hatarishi. Sisi ni viongozi wa kusimamia Serikali hivyo tutaenda kuishauri Serikali yetu ili tuweze kuwa na namna bora ya kuchoma taka hatarishi kama tulivyojifunza hapa”. amesema Mhe. Mtumwa.

Naye Bi.Maimuna Salum Mkurugenzi  wa Mazingira na taka hatarishi Tindwa Medical and Health service, amesema kuwa kiwanda kinafanya kazi kwa kushirikiana na Taasisi za Kiserikali ikiwemo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, TMDA, OSHA pamoja na NEMC ili kuweza kufanya kazi zao kwa uweredi na kuzingatia matakwa ya Sheria ya Nchi. 

Ameeleza kuwa Tindwa inajishughulisha na uteketezaji wa taka hatarishi kutoka Hospitali na Viwandani na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuteketeza taka japo changamoto waliyonayo kwa sasa ni baadhi ya kemikali kushindwa kuteketezwa kutokana na uwezo mdogo wa mashine walizonazo. Aidha ameeleza kuwa kila penye changamoto fursa ipo hivyo kama kiwanda wamejipanga kuongeza uwezo wa mashine ambazo zitaweza kuteketeza taka hizo ambazo mashine ya sasa imeshindwa.

Previous articleMAJALIWA AKAGUA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA KATAVI
Next articleAFISA MADINI KUMBURU ATATUA MGOGORO YA WACHIMBAJI NA KUWAONYA KUTOKUPELEKA KESI MAHAKAMANI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here