Afisa Mfawidhi Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Tullo Masanja,akizungumza wakati wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipo fanya ziara ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Anaripoti: Alex Sonna, Fullshangwe Blog, DODOMA.
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imetembelea Makao ya Taifa ya watoto Kikombo nje kidogo ya Jiji la Dodoma huku ikiridhishwa na huduma bora zinazotolewa kwa watoto wa mitaani waliopo katika kituo hicho.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Stanslaus Nyongo, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya Jiji la Dodoma,amesema kuwa wameridhishwa na usimamizi mzuri uliopo.
”Kwa kweli sisi kama Kamati tumeridhishwa na malezi mnayoyatoa kwa watoto hawa hivyo tunaishauri Serikali kuendelea kuwakusanya watoto wa mitaani walipo katika maeneo mbalimbali nchini na kuwaweka katika vituo ili kuwapatia mahitaji yao ya msingi”amesema Nyongo
Nyongo amesema kutokana na kituo hicho kuwa na uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 250, jitihada za kuwakusanya na kuwaleta watoto kutoka maeneo mbalimbali zinatakiwa kufanyika.
“Niendelee kuwasihi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuendelea kuwaleta watoto wa mitaani katika vituo kama hivi ili waje wapate huduma zinazotolewa kwani tatizo hili bado kubwa sana huko mtaani.
“Taarifa yenu inadai kuwa hadi sasa kuna watoto 54 lakini kituo hichi kina uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 250, hivyo kamati inaagiza kuleta wengine ikiwemo wale kutoka kituo cha Kurasini Dar es saalam waje hapa na waondolewe kule ambako mazingira siyo mazuri kama ilivyo hapa”amesema Nyongo.
Aidha, amesema kutokana na kituo hicho kuwa cha kipee Serikali inatakiwa kuweka nguvu kwenye maslahi ya watumishi wanao hudumia watoto.
“Kituo hichi ni cha kipekee hivyo watumishi waliopo hapa mnatakiwa kuwaangalia sana hasa katika maslahi yao kama maslahi yao yatakuwa wasiwasi basi hata watoto hawa watakuwa katika malezi yasiyofaa,”amesema.Nyongo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itasimamia Makao hayo ili yaweze kutoa huduma kwa Watoto waliokusudiwa kulelewa hapo.
Waziri Dkt Gwajima ameongeza kuwa, watoto kulelewa kwenye makao ni hatua ya mwisho kabisa baada ya kushindikana kuishi kwenye familia zao na kuwataka wazazi kuacha kuwatelekeza watoto wao hali inayowafanya kukimbilia mitaani.
“Nina imani ziara hii imewapa picha ya nini kinaendelea katika ulimwengu wa watoto wanaoishi mtaani hapa nchini na Serikali inafanya nini kukabiliana na hali hii, pia imewapa picha kwamba changamoto bado ni kubwa nchini, huu ni mtihani wa Taifa na Wizara, hivyo Serikali haiwezi kufanya peke yake. Nichukue fursa hii kutambua mchango wa ABBOTT FUND, tunahitaji kuimarisha ushirikiano na wadau hawa,” aliongeza Mhe. Gwajima.
Dkt. Gwajima ameihakikishia Kamati pia kuwa ushauri uliotolewa na wabunge umepokelewa na kuahidi kuufanyia kazi kwa kuanza kuwasilisha mpango kazi mahususi utakaotumika kutekeleza maoni yaliyotolewa na wabunge hao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt.John Jingu amesema kituo hicho kimetumia zaidi ya Sh. bilioni 12, hadi kukamilika na kilianza kujengwa mwaka 2017 na kilizinduliwa June 16,2021 na Makamu wa Rais wa Tanzania,Dkt Philip Mpango
kwa niaba ya Shirika la ABBOTT FUND Mwakilishi wa Shirika hilo Natalia Lobue amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani katika mazingira magumu wanapata fursa ya kuishi pazuri na kupata elimu na malezi bora.
Kwa upande wake,Mjumbe wa Kamati hiyo Mbunge wa Viti maalum(CHADEMA) Salome Makamba, ameshauri kituo hicho pamoja na kutoa elimu kwa watoto pia kubuni mafunzo mengine ya ufundi na michezo ili kuibua vipaji.
Makamba amesema kuwa wanaamini hawa watoto wakifundishwa michezo tutawapata wakina Samatta na Msuma wengine kupitia Vituo hivi vinavyolea watoto wa mitaani hivyo nawashauri muanze kubuni fani mbalimbali.
“Ninashauri kituo hiki kuwekeza katika kubuni fani za ufundi ili watoto hawa wanapotoka hapa wawe na ujuzi lakini pia kwa wale wenye vipaji watafutiwe walimu wa michezo watakao kuwa wakiwafundisha”amesema Makamba.
Credit: Fullshangwe Blog.