NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Mkurugenzi mtendaji wa asasi kilele inayojishughulisha na kilimo cha horticulture yaani maua, mbogamboga, matunnda, viungo na mazao yatokanayo na mizizi (TAHA) Dkt Jacqueline Mkindi amewataka wanawake kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kujilinda kwaajili ya familia zao, jamii na taifa kwa ujumla kwani chanjo hiyo haina madhara.
Dkt Mkindi aliyasema hayo wakati aliposhiriki katika uzinduzi wa chanjo ya UVIKO-19 mkoa wa Arusha ambapo alisema kuwa wanawake wasiwe na hofu kwani wamefuatialia jambo hilo kitaalamu na kupata ushauri wa wataalamu hivyo wakachanje kwani wanawake wanakutana na mengi na yanawategemea wao ili kusonga mbele.
“Msisikilize mambo yanaongelewa mtaani, chukueni hatua sahihi mimi sijapata mabadiliko yoyote nimechanja, sisikii wala sioni mabadiko yoyote kwenye mwili wangu niko sawa kwahiyo ninawashauri kutokana na janga hili chukueni hatua ya kuja kuchanjwa,” Alisema Dkt Mkindi.
Alieleza kuwa kutoka na hali halisi nawashauri watanzania wenzangu akina mama, makundi maalum na wanaume hasa wafanyabiashara, wanaokutana na watu wengi, wanaosafiri kila sikukwaajili ya kujenga uchumi wa nchi kujitokeza kwasababu ndio mikakati ya kupambana na hali inayoendelea sasa hivi.
Kwa upande wake Violet Alex mdau wa masuala ya usafirishaji na utalii alisema kuwa baada ya kuchanjwa hajaona mabadiliko yoyote hivyo jamii ishiriki kikamilifu kwani walishashiriki chanjo nyingi tangu utotoni na hazijawaletea madhara yoyote hivyo watu waache kudanganya na kila mmoja afikiri kuhusu afya yake kwani ukiwa na maradhi huwezi kufanya shughuli za uzalishaji.
Aidha aliomba makampuni kushauri wafanyanyakazi wao kupata chanjo pamoja na watu wanaowazunguka kwani kwa kufanya hivyo itasaidia wageni wengi kuingia katika mkoa wa Arusha na kuweza kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Mmoja wa wananchi Honesta Alfayo mkazi wa jiji la Arusha alisema kuwa wamesikia maneno mengi kuhusiana na chanjo hiyo lakini yeye Kama mwananchi alishaona madhara yaliyoletwa na UVIKO-19 kwani ndugu jamaa na marafiki zao wamepoteza maisha kwasababu ya virusi hivyo wanaishukuru serikali kwa kuleta chanjo hiyo ambayo itasaidia kwa asilimia kubwa kuokoa maisha ya watu wengi.