Home LOCAL DITOPILE AWAVAA WANASIASA NA VIONGOZI WA DINI WANAOPOTOSHA KUHUSU CHANJO

DITOPILE AWAVAA WANASIASA NA VIONGOZI WA DINI WANAOPOTOSHA KUHUSU CHANJO

MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ametoa wito kwa Viongozi wa Dini, Wanasiasa na watu wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kuchoma chanjo.

Ditopile ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni siku kadhaa tangu kuwepo kwa baadhi ya wanasiasa na viongozi wa Dini ambao wameonesha mtazamo hasi kuhusu uchomaji wa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19.

Ditopile amesema ni vema viongozi hao kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ugonjwa huo kwa kuhamasisha wananchi kuwa na mapokeo chanya ya chanjo na kuacha kufanya upotoshaji.

Amesema Serikali ya Rais Samia kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa na Vyombo vingine, vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa chanjo za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani na kuwataka watanzania kuepuka uzushi wa wanasiasa wachache wenye maslahi binafsi kwenye suala la Chanjo.

“Kwenye Chanjo Serikali ya Rais Samia imeweka utaratibu mzuri sana wa kila mwananchi kupatiwa Chanjo bila usumbufu, utaratibu huu ni pamoja na kuainisha vituo, kuweka mfumo kwa kujisajili, kujaza fomu ya uhiari ya kupatiwa Chanjo na kupewa kadi kwaajili ya kumbukumbu baada ya kuchanja, niwahimize wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hii ambayo ni salama na imethibitishwa na wataalamu.

Lakini pia Serikali ya Rais Samia inaendelea na jitihada za kupambana na ugonjwa huu hatari wa Corona Juhudi mbalimbali zinachukuliwa kwa Mfano tumeona serikali imepunguza gharama za upimaji wa Ugonjwa wa UVIKO-19 Kwa wasafiri kutoka dola 100 Hadi dola 50 kwa kipimo Cha RT PCR,” Amesema Ditopile.

Amesema tangu aingie madarakani Machi mwaka huu Rais Samia ameonesha kupiga hatua kubwa za kimaendeleo ambapo kwenye sekta ya kilimo bei ya Alizeti imepanda kutoka Sh 500-1000 kwa kilo mwaka jana hadi Sh 950-1300 mwaka huu jambo ambalo limeoneza unafuu kwa wakulima.

Ditopile pia amepongeza jitihada za kuinua uchumi zinazofanywa na Serikali ambapo wiki hii Meli kubwa ya mizigo iliyobeba magari 3743 imetua nanga katika Bandari ya Dar es Salaam ikiweka rekodi ya kuwa Meli ya kwanza kushusha idadi kubwa ya magari Nchini.

Ameipongeza pia Serikali kwa kusikia kilio cha Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwa kutambua umuhimu wa kujenga uwezo wa TARURA katika kutimiza majukumu yake.

” Wabunge wote wa Majimbo wamepatiwa Sh Milioni 500 kwa ajili ya miundombinu ya barabara ya TARURA lakini TARURA itapatiwa magari 122 yote haya ni kuongeza ufanisi wao katika kutekeleza miradi ya barabara,” Amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here